Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Karibu

Wizara ya Katiba na Sheria ndiyo mhimili mkuu wa masuala yote ya kisheria nchini. Bila shaka ni kutokana na umuhimu huu, ndiyo sababu Wizara hii ikawa na umri wa miaka 55 sawa na umri nchi yetu hii leo.

Historia ya Wizara ilianza mwaka 1961 wakati Waziri Mkuu wakati huo, Hayati Julius Nyerere alipomteua Chifu Abdallah Fundikira kuwa Waziri wa Sheria wa Kwanza Mzalendo kabla nafasi hiyo kuchukuliwa na Sheikh Amri Abeid Kaluta mwaka 1963 na baadaye Mhe. Hassan Nassor Moyo kuanzia mwaka 1964 aliyeshika nafasi hiyo hadi 1966. Baada ya hapo shughuli za Wizara zilihamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Pili wa Rais chini Hayati Rashid Mfaume Kawawa.

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1975, Wizara na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ziliunganishwa kupitia Tangazo la Serikali Na. 10 la mwaka 1975 na Mhe. Jullie Manning aliteuliwa kuwa Waziri na Mwanasheria Mkuu wa Serikali hadi mwaka 1982 alipoteuliwa Mhe. Joseph Warioba kushika nafasi hizo. Utaratibu huu uliendelea hata baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1985 wakati Mhe. Damian Lubuva alipoteuliwa kushika nyadhifa hizo mbili hadi mwaka 1990.

Mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa mwaka 1990 yalipelekea Waziri na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutenganishwa tena na hivyo kofia ya Uwaziri na kofi ya Uanasheria Mkuu wa Serikali zikatofautishwa. Wakati huo, shughuli za Waziri zilihamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ikabaki kuwa Idara inayojitegemea chini ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais. Mabadiliko haya yalifanywa kupitia Tangazo la Serikali Na. 140 la mwaka 1990.

Mwaka 1993, Rais Alli Hassan Mwinyi aliirudisha tena Wizara ya Sheria na Mambo ya Katiba na kumteua Mhe. Samuel Sitta kuwa Waziri na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ikabaki kuwa Idara inayojitegemea chini ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, Rais Benjamin Mkapa aliendelea na Wizara hii kupitia Tangazo la Serikali Na. 720 la mwaka 1995 na kumteua Mhe. Harith Mwapachu kuwa Waziri. Katika muundo huu mpya, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilirudishwa chini ya Wizara hii kutoka Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na Katibu Mkuu wa Wizara akawa pia ndiye Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mwaka 2005, baada ya Uchaguzi Mkuu, Rais Jakaya Kikwete aliunda tena Wizara hii wakati huu ikiitwa Wizara ya Katiba na Sheria. Hata hivyo, ili kuongeza ufanisi, mwaka 2008 kufuatia mapendekezo ya Tume ya Jaji Mark Bomani, Wizara ilitenganishwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali hatua iliyopelekea pia kutenganishwa kwa nafasi ya Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali na ile ya Katibu Mkuu wa Wizara.