Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

MIFUMO 12 YA SHERIA ZA VIPAUMBELE KUFANYIWA MAREKEBISHO MWAKA 2026/27 KUTEKELEZA DIRA 2050

Imewekwa: 04 Sep, 2026
MIFUMO 12 YA SHERIA ZA VIPAUMBELE KUFANYIWA MAREKEBISHO MWAKA 2026/27 KUTEKELEZA DIRA 2050

Serikali imeanza  kufanyia marekebisho ya mifumo 12 ya sheria iliyobainika kuwa ya kipaumbele katika mwaka huu wa fedha, ikiwa ni  juhudi za kuweka mazingira wezeshi ya kisheria kwa uwekezaji, biashara na maendeleo ya huduma za jamii, kwa mujibu wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.

Hayo yameelezwa leo  Septemba 04, 2026, Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Katimba, wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Mbarali, Mhe. Bahati Kenneth Ndingo, aliyeuliza namna Serikali ilivyojipanga kupitia na kuwasilisha Bungeni mabadiliko ya sheria zinazoweza kuwa kikwazo katika utekelezaji wa Dira hiyo.

Naibu Waziri amesema Serikali inaendelea kupitia sheria mbalimbali nchini kwa lengo la kubaini na kuondoa vifungu au masharti ya kisheria yanayoweza kukwamisha utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.

Amesema zoezi hilo linatokana na agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alilolitoa wakati wa uzinduzi wa Dira 2050, akielekeza Wizara ya Katiba na Sheria, kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Tume ya Marekebisho ya Sheria Tanzania, kufanya tathmini ya sheria na kupendekeza maboresho yanayohitajika.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri, Serikali tayari imeandaa mpango wa kupitia mifumo 28 ya sheria, huku zoezi likiendelea katika maeneo ya viwanda, biashara, uwekezaji, kodi na nishati.

Akijibu swali la nyongeza la Mhe. Ndingo kuhusu hatima ya sheria zinazohusu kilimo na maendeleo ya jamii, amesema vipaumbele vyote vya Dira 2050 vinazingatiwa katika zoezi hilo, ikiwemo kilimo, usalama wa chakula na rasilimali watu.

Amesema sekta binafsi inatarajiwa kuchangia asilimia 70 ya uwekezaji katika utekelezaji wa Dira 2050, hivyo Serikali inaendelea kuhakikisha kuwa kunakuwa na mfumo wa sheria unaoweka mazingira rafiki kwa sekta hiyo na kuchochea uwekezaji pamoja na shughuli za kiuchumi.

Marekebisho hayo yanalenga kuhakikisha kuwa sheria zinaendana na mahitaji ya utekelezaji wa Dira 2050, kurahisisha uwekezaji, biashara na uzalishaji, pamoja na kuondoa vikwazo vya kisheria vinavyoweza kuchelewesha maendeleo ya Taifa.

Serikali imesisitiza kuwa itaendelea kutekeleza zoezi hilo kwa kuzingatia vipaumbele vilivyowekwa, ili maboresho ya sheria yakamilike kwa wakati na kuwawezesha wananchi kunufaika na fursa zitakazotokana na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.