Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

ZINGATIENI MASHARTI YA AJIRA ILI KUPATA HAKI ZENU-DKT. HOMERA

Imewekwa: 24 Aug, 2026
ZINGATIENI MASHARTI YA AJIRA ILI KUPATA HAKI ZENU-DKT. HOMERA

Watumishi wametakiwa kufahamu na kufuatilia haki na stahiki zao za msingi wakati wote wa ajira, huku wakisisitizwa umuhimu wa kutunza nyaraka zinazoweza kutumika kama ushahidi katika kudai haki zao.

Wito huo umetolewa leo 24 Agosti, 2026 na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Juma Homera wakati akitoa elimu ya ajira na mafao wakati wa programu ya Sema na Waziri inayoratibiwa na wizara kupitia kituo cha huduma kwa mteja.

Dkt. Homera amesema wafanyakazi wanapaswa kuzingatia masharti ya ajira zao ikiwemo mikataba na barua za ajira, kumbukumbu za mishahara na malipo, muda wa kazi na wajibu wao, barua za uhamisho pamoja na mawasiliano muhimu kati yao na waajiri, kwa kuwa nyaraka hizo ni sehemu muhimu ya ushahidi pale yanapotokea madai au migogoro ya ajira.

“Ni muhimu mfanyakazi kuwa na nyaraka na ushahidi wa stahiki zake pamoja na kufanya ufuatiliaji wa michango yao mara kwa mara jambo litakalowasaidia kuwa na taarifa sahihi pale wanapofuatilia haki zao kwenye mamlaka husika,” amesema Dkt. Homera.

“Miongoni mwa malalamiko tunayoyapokea kupitia programu hii yanayowahusu watumishi ni pamoja na kutokulipwa mshahara kwa miezi kadhaa, mishahara ya vipindi vya nyuma ambayo haijalipwa, madai ya fedha kutokana na uhamisho, gharama za safari za kazi na madai yaliyobaki baada ya kuacha au kustaafu kazi, nitoe wito kwa watumishi kuhakikisha wanatunza nyaraka zao ili kuepuka kupoteza haki zao wanapomaliza au kuacha kazi na wakati wa kuhama” amesisitiza Dkt. Homera.

Aidha, Dkt. Homera amewataka watumishi kutafuta ushauri wa kisheria na kufuata taratibu zilizowekwa pale wanapoona haki zao hazijatekelezwa kwa kuwa migogoro ya ajira ina mamlaka na taratibu zake kulingana na aina ya mgogoro.

Programu ya Sema na Waziri imelenga kumpa fursa mwananchi kupiga simu na kuwasilisha changamoto, maoni au ushauri moja kwa moja kwa Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria na kupatiwa ufumbuzi.