Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Balozi Dkt. Chana Afanya Mazungumzo na Balozi wa Uingereza

Imewekwa: 31 Jan, 2024
Balozi Dkt. Chana Afanya Mazungumzo na Balozi wa Uingereza

Na William Mabusi – WKS Dodoma

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Mhe. Balozi David Concar tarehe 31 Januari, 2024 Ofisi za Bunge Dodoma.

Mazungumzo hayo yalilenga kuweka vipaumbele vya mradi mpya wa BSAAT unaotarajiwa kuanza baadaye mwaka huu baada ya mradi unaoendelea kuisha muda wake. Katika kikao hicho Dkt. Chana kupitia Ubalozi wa Uingereza nchini, ameishukuru Serikali ya Uingereza kwa ufadhili wa mradi huo ambao pamoja na masuala mengine umesaidia kuleta mapinduzi makubwa katika kupambana na rushwa nchini, utungaji wa Kanuni za Kuwalinda Watoa Taarifa na Mashahidi, 2023, ujenzi wa Kituo cha kupokea taarifa na malalamiko.

Dkt. Chana ametaja maeneo ya kipaumbele kwenye mradi ujao kuwa ni pamoja na kuimarisha ofisi na vitendea kazi kwenye Wizara na Taasisi za haki jinai, kufanya marekebisho ya Sheria ya Kuwalinda Watoa Taarifa na Mashahidi (Whistle Blower Act, 2015), kujenga uwezo kwenye uandaaji wa miswada ya kisheria na mikataba hususan ya ulinzi wa maliasilia za nchi, kuwajengea uwezo Waendesha Mashtaka na Wachunguzi wa makosa ya jinai ili kupambana na mbinu mpya za uhalifu.

Akiongea katika kikao hicho Mhe. Balozi Concar amesema Serikali ya Uingereza itaendelea na ufadhili wa mradi wa BSAAT kuunga jitihada za Serikali katika kupambana na rushwa, Ukatili wa kijinsia  na watoto na utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai.