Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Bunge laridhishwa na Utekelezaji wa Mapendekezo Inayotoa kwa Serikali

Imewekwa: 13 Feb, 2024
Bunge laridhishwa na Utekelezaji wa Mapendekezo Inayotoa kwa Serikali

Na William Mabusi – WKS Dodoma

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Joseph Mhagama amesema Bunge linaridhishwa jinsi Serikali inavyotekeleza ushauri na mapendekezo yanayotolewa na Bunge kupitia Kamati mbalimbali za Kudumu.

Dkt. Mhagama amesema hayo leo tarehe 13 Februari, 2024 alipokuwa anasoma Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria katika kipindi cha kuazia Februari, 2023 hadi Januari, 2024. Kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge husimamia utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Wizara tano ikiwemo Wizara ya Katiba na Sheria.

“Kwa sehemu kubwa, Kamati imeridhishwa na utekelezaji wa maazimio ya Bunge uliofanywa na Wizara na taasisi zake. Kwa yale maeneo ambayo yanahitaji kutiliwa mkazo zaidi katika utekelezaji wake, Kamati imetoa ushauri mahsusi ili yakafanyiwe kazi zaidi.” Alisema.

Ameyataja mapendekezo hayo kuwa ni pamoja na Serikali kuendelea kuboresha majengo ya Mahakama za Mwanzo yanayostahili kuboreshwa ama kujenga mapya na kuwekwa miundombinu ya TEHAMA itakayowezesha Mahakama hizo kutoa huduma za TEHAMA kama ilivyo kwenye Mahakama zingine, Serikali kuendelea kuboresha miundombinu ya Taasisi za mfumo wa Haki Jinai na kuajiri watumishi wa kutosha kwenye Taasisi hizo kwa kuzingatia Ikama.

Akijibu mapendekezo hayo kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda amesema Serikali kwa kushirikiana na Mahakama inaendelea na Mpango wa ujenzi wa majengo ya Mahakama za Mwanzo katika maeneo mbalimbali nchini ili kusogeza huduma karibu na wananchi. Chini ya Mpango huo katika mwaka wa fedha 2023/24 zinajengwa Mahakama za Mwanzo 72 katika mikoa mbalimbali. Aidha, kwa kuzingatia Mpango wa Ujenzi wa Mahakama, mwaka wa fedha 204/25 Mahakama za Mwanzo 32 zinatarajiwa kujengwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Akijibu pendekezo la kuwekwa miundombinu ya TEHAMA kwenye Mahakama za Mwanzo, Mhe. Pinda amesema majengo mengi ya Mahakama za Mwanzo yapo maeneo ambayo hayajafikiwa na mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, na hivyo kushindwa kuunganishwa kwenye miundombinu ya moja kwa moja. Kwa sasa katika kukabiliana na changamoto hiyo, Mahakama imetengeneza mfumo maalum wa Mahakama za Mwanzo (Primary Court Mobile App) ambao unawezesha kutunza takwimu na kumbukumbu za mashauri yanayoendeshwa katika Mahakama hizo.

Kuhusu mapendekezo ya Serikali kuendelea kuboresha miundombinu ya Taasisi za mfumo wa Haki Jinai amesema Serikali itaendelea kuomba ongezeko la bajeti na ongezeko la watumishi katika taasisi hizo kwa ajili ya kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Kipindi hicho jumla ya miswada 12 ilichambuliwa na Kamati kutoa mapendekezo ya Bunge, Kamati ilitembelea na kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotengewa fedha katika Mwaka wa Fedha 2022/2023. Aidha, Kamati ilifanya uchambuzi wa utekelezaji wa Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na kujiridhisha na matumizi ya bajeti hizo.