Busara, Uvumilivu na Hekima Zitumike Kutoa Huduma za Msaada Wa Kisheria

Watoa Huduma za Msaada wa Kisheria wa Kaskazini Unguja wameaswa kutumia busara, uvumilivu na hekima wakati wa kutoa huduma hizo katika ngazi ya shehia.
Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Bi. Hanifa Ramadhani ametoa wito huo wakati akifungua mafunzo kwa watoa huduma za Msaada wa Kisheria mkoani Kaskazini Unguja, Aprili 22, 2025.
Amesema Wizara imeandaa mafunzo ya siku moja ili kufanikisha utekelezaji wa kampeni ya Msaada wa kisheria ya Mama Samia mkoani humo kwa kuwajengea uwezo watoa huduma hao.
"Lengo la mafunzo haya kwanza ni kuwajengea uwezo wa namna kampeni hii inavyotekelezwa lakini pia tunabadilishana uzoefu na matarajio yetu ni mtoe huduma za Msaada wa kisheria kwa ufanisi mkubwa", amesisitiza Ramadhani.
Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Afisa Utumishi Mboja Hisabu Ali amesema Mkoa utatoa ushirikiano wa kutosha katika utekelezaji wa kampeni hiyo na kwamba Mkoani hapo kuna amani na utulivu hivyo watoa huduma watafanya kazi yao bila matatizo.
"Ninapenda kuwakaribisha sana mkoa wa Kaskazini Unguja huku kuna amani ya kutosha na tunaahidi kutoa ushirikiano wa hali ya juu ili kufanikisha utekelezaji wa kampeni hii", amesisitiza Ali.
Kwa upande wake Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria (Bara) Edith Shekidele amesema ushirikiano wa Tanzania Bara na Zanzibar umeanza tangu kuandaa mkakati wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia hadi sasa wakati wa utekelezaji wake.
Shekidele amesema "kilichofanyika Bara ndicho kinafanyika na huku Kaskazini Unguja na lengo kuu la mafunzo haya tunabadilishana uzoefu wa namna tunavyotekeleza kampeni hii".
Uzinduzi wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria Kaskazini Unguja unatarajiwa kufanyika kesho tarehe 23 Aprili 2025 katika uwanja wa Tumaini Skuli ya Mkwajuni.