Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Cheti cha Kuzaliwa Sio Kigezo Pekee cha Uraia

Imewekwa: 27 Jan, 2024
Cheti cha Kuzaliwa Sio Kigezo Pekee cha Uraia

Na Lusajo Mwakabuku - Njombe

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema cheti cha kuzaliwa hakimpi mtu yeyote uhalali wa uraia wake bali ni uthibitisho wa kuzaliwa kwake au kinaweza kutumika kama moja ya kigezo cha kuthibitisha uraia.

Waziri Dkt. Pindi Chana ameyasema hayo wakati alipotembelea Ofisi za Msajili wa Vizazi na Vifo Mkoa wa Njombe kwa lengo la kuangalia hali uandikishaji usajili wa watoto chini ya miaka mitano, tarehe 27 Januari, 2024.

“Sio uthibitisho pekee na ndiyo maana cheti cha kuzaliwa hata mtoto ambaye wazazi wake wote wawili sio watanzania ni wageni wamekuja kutalii akizaliwa Tanzania atapata cheti hivyo katika vigezo vyetu vya kuangalia huyu ni Mtanzania ama sio Mtanzania cheti cha kuzaliwa kinaweza kikatumika lakini sio guarantee pekee,” alisema Dkt. Chana.

Alisema kuwa cheti cha kuzaliwa kinathibitisha kwamba mtu huyu ni mzaliwa nchini Tanzania lakini sio hakikisho la mwisho kwamba wewe ni mzawa.

“Tukija kwenye utaratibu wa uraia kuna taratibu zake, kuna sheria zake za kutambua kwamba huyu je ni Mtanzania au sio Mtanzania hivyo niwakumbushe cheti cha kuzaliwa kinaonyesha mtoto amezaliwa wapi na habari za uraia kuna taratibu nyingine,” alisema Dkt. Chana.

Balozi Dkt. Chana alisema kila mtoto Mtanzania anapozaliwa anayo haki ya kupata cheti cha kuzaliwa kwa sababu ni haki ya kila mmoja.

“Watanzania wenzangu, wamama wenzangu tunapokwenda katika zahanati, hospitali na hivi sasa tupige marufuku kabisa watu kujifungulia nyumbani, watu wanatakiwa kujifungulia katika vituo vya afya tumejenga tunavyo vya kutosha na hivyo mtoto anapozaliwa hakikisha kabla ya kuondoka kwenda nyumbani unapata cheti chako cha kuzaliwa cha mtoto,” alisema Waziri Chana.

Alisema Serikali imedhamiria kwamba tangu mwaka 2020 hadi 2025 kila mtoto anayezaliwa na watoto wote wanatakiwa kuwa na vyeti vya kuzaliwa.

“Tatizo ni nini Watanzania wenzangu, shida ni nini ni haki yako chini ya umri wa miaka mitano tena unapata bure Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ameshafadhiri lakini wale wa umri ambao umezidi miaka mitano pia cheti cha kuzaliwa ni haki yako lakini kuna malipo kiasi fulani kidogo ambacho unapaswa kulipa ili upate cheti chako,” alisema.

Pia waziri amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha kwamba wanatenga fedha kwa ajili ya kuwezesha shughuli za usajili wa watoto chini ya miaka mitano.

Awali Mratibu wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini RITA Mkoa wa Njombe, Rahabu Daud alisema mpango wa usajili wa watoto chini ya miaka mitano katika mkoa wa Njombe ulianza kutekelezwa kuanzia Septemba 2016 hadi hivi sasa jumla ya watoto 190,075 wamesajiliwa na kupatiwa vyeti hadi kufikia Januari 25 mwaka 2024.

“Watoto hawa waliosajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa wakati wakiwa na umri wa chini ya miaka mitano na kiwango cha usajili katika mkoa kimeongezeka kutoka asilimia 8.6 (Sensa 2012) hadi kufikia asilimia 64.9 Januari 2024,” alisema Daud.

Alisema kabla ya kutekeleza mpango huo Halmshauri za wilaya za Njombe, Ludewa na Wanging’ombe hali ya usajili ilikuwa asilimia sita mwaka 2012 na kufikia Januari 2024 hali ya usajili umeongezeka kwa wastani wa asilimia 65.