Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Dkt. Chana Afanya Mazungumzo na Balozi wa Singapore Nchini

Imewekwa: 21 Nov, 2023
Dkt. Chana Afanya Mazungumzo na Balozi wa Singapore Nchini

Na William Mabusi – WKS Dodoma

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amekutana na Balozi wa nchi ya Singapore nchini Mhe. Balozi Douglas Foo na kufanya mazungumzo kuhusu kuimarisha ushirikiano kwenye sekta mbalimbali na namna ya kubadilishana uzoefu kwenye masuala ya teknolojia.

Kikao hicho kimefanyika tarehe 20 Novemba, 2023 ofisi za Wizara Mtumba kwa lengo la kuendeleza ushirikiano baina ya nchi mbili hizo.

“Kama Wizara maeneo ya kubadilishana uzoefu ni kwenye sekta ya sheria, kuendeleza watumishi kwenye mafunzo mbalimbali. Aidha, tunaangalia namna ya kuimarisha ushirikiano wa kibiashara.” Alisema Dkt. Chana.

Katika kusimamia utawala wa sheria, Dkt. Chana amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea na jitihada za kuongeza uelewa wa sheria kwa wanachi na hasa wa hali ya chini kwa kuwapa elimu na huduma za kisheria kwa wasioweza kumudu gharama za Mawakili kupitia kampeni ya kitaifa ya mama Samia.

Katika hatua nyingine Dkt. Chana amesema Serikali imekuwa ikisisitiza wananchi kutatua migogoro kwa njia mbadala ya maridhiano ambako huokoa muda kwani mashauri humalizika kwa haraka bila wahusika kufikishana mahakamani.

Kwa upande wake Balozi wa Singapore amesema nchi yake itaendelea kuenzi uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi yake na Tanzania na kusema kuwa Singapore iko tayari kuingia makubaliano ya kibiashara na Tanzania, miongoni mwa mengine.