Dkt. Chana Aipongeza NPS kwa Utendaji Kazi
Na William Mabusi – WKS Dodoma
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) ametembelea Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) na kupokea tarifa ya utekelezaji ya mwaka wa fedha 2022/23 na kuipongeza kwa utekelezaji wa majukumu yake ya usimamiaji haki nchini.
Dkt. Chana akiwa ameongozana na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul (Mb), SACP Neema Mwanga aliyemwakilisha Katibu Mkuu amekutana na Menejimenti na watumishi wa ofisi ya NPS tarehe 02 Novemba, 2023 kwenye ofisi za Taasisi hiyo Jijini Dodoma.
“Tanzania si tu ina Mahakama lakini pia mtu ana uhakika wa kupatikana kwa haki yake na kwa wakati kwani tunashuhudia wenyewe kuongezeka kwa kasi ya kutoa maamuzi ya mashauri mbalimbali kwenye Mahakama zetu,” alisema Dkt. Chana.
Akiongelea kuhusu ushirikiano mzuri uliopo kati ya NPS na Ofisi zingine za Kikanda na Kimataifa ameitaka ofisi hiyo na Taasisi zingine za Wizara kutumia mwonekano wa nchi yetu kimataifa wa kusimamia na kuimarisha haki za binadamu kutafuta Wadau wengi wa Maendeleo watakaosaidia kufadhili utekelezaji wa miradi mbalimbali.
“Pamoja na jitihada za Serikali za kukabiliana na changamoto mbalimbali kwenye Taasisi zake bado natoa wito tuongeze ushirikiano na Wadau wa Maendeleo. Kuna baadhi ya nchi vipaumbele vyao ni haki za binadamu hivyo kwa kuwa tunasifika kama nchi inayozingatia utawala wa sheria, nchi kama hizo ndizo za kushirikiana nazo. Ushirikiano huo utatuwezesha kukabiliana na changamoto kama upungufu wa vitendea kazi, mafunzo ya teknolojia kwenye sekta mbalimbali na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.” Alisema.
Aidha, Dkt. Chana ameunga mkono uamuzi wa wafungwa kuhusishwa kwenye shughuli za uzalishaji katika kilimo na shughuli zingine za maendeleo, “Magereza yawe na mashamba kwa ajili ya kilimo ili tusije kuwa tunachukua pesa ya mtenda haki kwenda kulisha mhalifu, na kila mnapowatembelea ‘maana ni jukumu lenu pia’ wakumbusheni kuwa wao ni watanzania wenzetu na kuwahimiza kuacha uhalifu ili wawe raia wema watakapomaliza vifungo vyao.”
Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji, Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu ameshukuru na kupongeza lengo la Serikali la kufungua ofisi za Mashtaka katika kila Wilaya nchini ambapo hadi sasa bado Wilaya 47. Aidha, amesema NPS kama kiungo kikubwa katika mnyororo wa haki jinai wataendelea kushirikiana na vyombo vingine vya uchunguzi kusimamia haki na wataendelea kusimamia mashirikiano mazuri ya kikanda na kimataifa kwenye masuala ya jinai.