Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Dkt. Kazungu Akutana na Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola

Imewekwa: 02 Oct, 2023
Dkt. Kazungu Akutana na Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola

Na William Mabusi – WKS Dodoma

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Khatibu Kazungu amekutana na kufanya mazungumzo na ugeni kutoka Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola ukiongozwa na Katibu Mkuu Msaidizi wa Jumuiya ya Madola Prof. Luis Gabriel Franceschi  kwa lengo la kushirikiana  katika Maandalizi ya Mkutano wa Mawaziri wa Sheria wa Jumuiya hiyo utakaofanyika  nchini Tanzania, Zanzibar   tarehe 4 hadi 8  Machi, 2024.

Majadilino hayo yamefanyika  tarehe 02 Oktoba, 2023 katika  ukumbi wa mikutano wa Wizara ulioko Mji wa Serikali Mtumba Dodoma. Katika mkutano huo ambao pia Menejimenti ya Wizara ilihudhuria, mambo mbalimbali yamejadiliwa kuhakikisha mkutano huo unafanyika katika mazingira mazuri, Naibu Katibu Mkuu ameihakikishia Sekretarieti hiyo kuwa Tanzania iko tayari  na imeanza  maandalizi ya Mkutano wa Mawaziri wa Sheria wa Jumuiya ya Madola.

Katika mkutano huo nchi 56 wanachama wa Jumuiya ya Madola zinatarajiwa kuhudhuria, mkutano kama huu mara ya mwisho umefanyika Mauritius mwaka 2022.