DKT. HOMERA ATAKA SHERIA MAHSUSI KULINDA BIASHARA MTANDAO
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Homera, ametoa wito kwa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kufanya utafiti kuhusu uanzishwaji wa Sheria mahsusi ya Biashara Mtandao (E-Commerce Law) kwa lengo la kuweka mazingira ya kisheria yaliyo salama, rafiki na yenye uhakika kwa biashara na uwekezaji wa kidijitali, kukuza ubunifu na ushindani, kulinda wafanyabiashara pamoja na kuiwezesha nchi kutumia kikamilifu fursa zinazotokana na ukuaji wa uchumi wa kidijitali.
Dkt. Homera ametoa wito huo 2 Septemba, 2026, jijini Dar es Salaam wakati wa kikao cha kujadili hatua zilizofikiwa katika maboresho ya sheria kwa ajili ya kuweka mazingira wezeshi ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kilichowakutanisha Waziri wa Katiba na Sheria na Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Bw. George Nathaniel Mandepo.
“Kutokana na mabadiliko ya teknolojia, kukua kwa Uchumi wa kidijitali pamoja na kuongezeka kwa biashara mtandao kuna umuhimu sasa wa kuwa na mfumo wa kisheria unaoendana na mazingira ya sasa na yanayotarajiwa ya uchumi wa kidijitali’’ alisema Dkt. Homera.
“Sambamba na hatua nyingine zinazochukuliwa na Serikali katika kuimarisha uchumi wa kidijitali, mnapaswa kuanza kufanya utafiti na kuwasilisha mapendekezo yatakayoiwezesha Serikali kufanya uamuzi wa kisera na kisheria kuhusu haja ya kutungwa kwa Sheria mahsusi ya Biashara Mtandao au kufanya maboresho stahiki katika sheria zilizopo’’ aliongeza Dkt. Homera.
Dkt. Homera alisema utafiti huu unatarajiwa kuchambua sheria zilizopo, kubaini changamoto za kisheria, pamoja na kufanya ulinganisho na mifumo ya sheria na uzoefu wa nchi nyingine katika kusimamia biashara mtandao.
Aidha, Dkt. Homera amebainisha kuwa hatua hii ya utafiti ni sehemu ya jitihada za kuendelea kuimarisha mfumo wa kisheria unaoendana na mabadiliko ya teknolojia, pamoja na kuweka mazingira bora kwa ukuaji wa biashara na uchumi wa kidijitali katika sekta zote ikiwemo sekta ya biashara yam azo ya kilimo nchini.
Maeneo yanayotarajiwa kupewa kipaumbele katika utafiti huo ni pamoja na mikataba ya kielektroniki, ulinzi wa watumiaji, usimamizi wa majukwaa ya kidijitali, malipo ya kielektroniki, ulinzi wa taarifa binafsi, usalama wa miamala, haki miliki, masuala ya kodi, ushindani pamoja na utatuzi wa migogoro ya biashara mtandao.