HOMERA: HAKUNA TAIFA IMARA BILA SHERIA IMARA
Makamishna wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, wametakiwa kutumia uzoefu na maarifa waliyonayo kuhakikisha Taifa linakuwa na sheria bora zitakazosaidia katika kutekeleza Dira 2050.
Hayo yamewekwa bayana na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera wakati akifungua mafunzo elekezi kwa Makamishna wapya wa ofisi ya Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania yaliyofanyika leo 01 Septemba, 2026, jijini Dodoma
Dkt. Homera amesema serikali imekua ikikutana na changamoto ya utekelezaji wa sheria ambazo hazijafanyiwa utafiti, jambo linalopelekea kuwa na sheria zilizopitwa na wakati na kuzitaka wizara na taasisi kabla ya kutunga au kubadili sheria kushirikiana na Tume kabla ya kuwasilisha mapendekezo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali au Mwandishi Mkuu wa Sheria.
Waziri Homera amesema hakuna Taifa imara bila kuwa na sheria imara na zenye tija kwa Taifa, na amewapongeza Makamishna waliomaliza muda wao na kuwataka Makamishna wapya kumsaidia Mhe. Rais katika kuhakikisha Sheria za Nchi zinaendana na wakati hasa katika kutekeleza Dira 2050.
Awali, akimkaribisha Mhe. Waziri, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Mhe. Jaji Winfrida Korosso, amesema Tume imejipanga vyema kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuishukuru Wizara kwa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu ya Tume, hatua iliyowezesha ufanisi wake.
Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania imeundwa chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania sura 171 na majukumu yake yameainishwa katika kifungu cha 4 cha sheria hiyo ikiwa na lengo la kuhakikisha nchi inakuwa na sheria himilivu na zinazoakisi mazingira ya Tanzania.