Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Gekul Ashiriki “Utu Kwanza Run” Dar es Salaam

Imewekwa: 10 Sep, 2023
Gekul Ashiriki “Utu Kwanza Run” Dar es Salaam

Na. Lusajo Mwakabuku – WKS Dar es salaam.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul akimwakilisha Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, ameungana na Wakimbiaji, Watembeaji na Waendesha Baiskeli walioshiriki “Utu Kwanza Run” tarehe 10 Septemba, 2023 Jijini Dar es Salaam.

Mbio hizo zilizoandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali (NGO) la Utu Kwanza, chini ya Uenyekiti wa Wakili Shehzada Amir Walli zimelenga kujitoa kwa hali na mali katika kutekeleza jukumu la kuboresha maisha ya Mahabusu na Wafungwa, familia za hao Mahabusu na Wafungwa, pamoja na kuangalia namna bora ya kuboresha maisha ya Maofisa wa Magereza wanaoishi na kuwajibika moja kwa moja na usimamizi wa Mahabusu na Wafungwa nchini.

Akiongea katika hafla hiyo, Gekul amesema malengo ya Utu Kwanza yanakwenda sambamba na maono ya Serikali ya Awamu ya Sita kwani Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kujali utu, aliunda tume maalum ya kupitia na kutoa mapendekezo ya kurekebisha mfumo wa haki jinai nchini ambayo imefanya kazi kubwa kwa kuzunguka nchi nzima ikikusanya mawazo kwa Wananchi na Wadau wote wa Sheria ili kuboresha Mfumo mzima wa Haki Jinai Nchini.

“Ndio maana, sisi kama Wizara ya Katiba na Sheria, hatukusita kupokea wito na kushiriki kwenye Hafla hii ya Utu Kwanza baada ya kuridhishwa na Malengo na kazi nzuri inayofanywa na Shirika hili la Utu Kwanza sambamba na jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha maisha ya Watanzania wote bila kujali rangi, itikadi, jinsia wala asili kwenye Sekta ya Upatikanaji wa Haki, na hasa Haki Jinai – ambako ndiko linapopatikana kundi la mahabusu na wafungwa.” Alisema Gekul.

Aidha Mhe. Gekul alitumia nafasi hiyo kuyataka mashirika mengine yanayojihusisha na utoaji wa msaada wa kisheria kutumia rasilimali zao vizuri ili kuwafikia walengwa na kushirikiana na Serikali katika kuboresha maisha ya watu wote huku akitaja utu kuendelea kuwa kipaumbele kwenye HAKI JINAI na na kuhakikisha wote tunatimiza wajibu wetu katika kuwatumikia Watanzania na kudumisha amani na mshikamano ambazo ni tunu muhimu kwa maendeleo na ustawi wa Taifa letu.

Pia Gekul amewapongeza Utu Kwanza kwa kuanzisha Mradi wa Dawati la Msaada wa Sheria, (LEGAL AID DESK) akisema kuwa dawati hilo licha ya kupokea changamoto mbalimbali za kisheria pia litatumika kama chanzo kingine cha fedha kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wengine.

“Mradi huu ukisimamiwa vizuri, utakuwa ni jawabu zuri kwa Umma na Watanzania walio wengi wanaohitaji msaada wa dharura hasa pale wanapopatwa na matatizo ya kijinai. Watanzania na Jamii, watumie fursa hizi vizuri ili watu wasio na uwezo wa kupata msaada wa kisheria kwa gharama za kulipia, wapate msaada unaostahili,” aliongezea Mhe. Gekul.