Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

SERIKALI YATUMIA BILIONI 524.9 KUBORESHA MIUNDOMBINU YA MAHAKAMA

Imewekwa: 01 Sep, 2026
SERIKALI YATUMIA BILIONI 524.9 KUBORESHA MIUNDOMBINU YA MAHAKAMA

Serikali ya Awamu ya Sita, kupitia Mhimili wa Mahakama, imechukua hatua mathubuti za kuboresha miundombinu ya utoaji haki nchini, ambapo zaidi ya Shilingi Bilioni 524.9 zimetumika katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Akijibu maswali ya wabunge wakati wa kipindi cha maswali na majibu wakati wa Bunge la Kumi na Tatu, Mkutano wa Nne, Kikao cha Nnecha  Bungeni Jijini Dodoma, 31 Agosti, 2026, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Katimba alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitano ilipita serikali imetumia fedha hizo kujenga majengo mapya ya mahakama pamoja na kukarabati majengo ya mahakama katika maeneo mbalimbali.

Aidha akijibu swali la Mbunge wa Urambo, Mhe. Margaret Sitta, aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itaanza ujenzi wa jengo jipya la Mahakama ya Mwanzo Wilaya ya Urambo, Naibu Waziri Katimba alieleza kuwa ujenzi wa majengo ya huduma za utoaji haki, ikiwemo mahakama za mwanzo na mahakama za wilaya, unaendelea kwa awamu nchini kote.

Mhe. Katimba alifafanua kuwa kwa Wilaya ya Urambo, Serikali imepanga kuanza ujenzi wa mahakama hiyo katika mwaka wa fedha 2027/2028.