Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

JAMII YATAKIWA KUTOFUMBIA MACHO UKATILI WA KIJINSIA

Imewekwa: 27 Aug, 2026
JAMII YATAKIWA KUTOFUMBIA MACHO UKATILI WA KIJINSIA

Jamii imetakiwa kutofumbia macho vitendo vya ukatili wa kijinsia na unyanyasaji wa kingono (GBV),msukumo ukitolewa  kwa mifumo ya utoaji haki nchini kuimarisha mwitikio wa kushughulikia  masuala hayo kwa wakati  kwa kuzingatia haki, utu na ulinzi wa manusura.

Wito huo umetolewa  Agosti 26, 2026, na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, wakati akizindua maonyesho ya shuhuda za manusura wa ukatili wa kijinsia yaliyofanyika katika viwanja vya Wizara, Mtumba jijini Dodoma.

Dkt. Homera amesema jamii ina wajibu wa kuchukua hatua dhidi ya ukatili wa kijinsia, huku akisisitiza mifumo ya sheria na mahakama kuendelea kutenda haki kwa kuzingatia mahitaji na maslahi ya manusura.

“Wito wangu kwa jamii ni kutofumbia macho masuala ya ukatili wa kijinsia, mifumo ya sheria na mahakama iendelee kuzingatia kutenda haki kwa mrengo wa manusura,” amesema Dkt. Homera.

Aidha, amewataka watoa huduma za msaada wa kisheria kuongeza wigo wa huduma hadi ngazi ya kata na vijiji ili wananchi wapate huduma hizo bila kujali wanapoishi. Pia amesisitiza jamii inayo  wajibu wa kuripoti matukio hayo ili wahusika wa vitendo vya ukatili wa kijinsia waweze  kuwajibishwa  kikamilifu  na kuchukuliwa  hatua za kisheria .

Kwa upande wake, Mshauri wa Masuala ya Kisheria wa GIZ, Tareq Bashour, amesema Programu ya SAFE inayotekelezwa na GIZ kwa kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria inalenga kuongeza uwezo wa wanawake na watoto kupata huduma za kisheria, hususan katika masuala yanayohusu  ukatili wa kijinsia.

Naye mwakilishi wa Mkurugenzi wa Women Action Towards Economic Development (WATED), Bi. Hamisa Rajabu, ameiomba Serikali kutazama uwezekano wa kuanzishwa kwa Baraza la Kitaifa la Manusura, litakalowapa nafasi manusura kushiriki katika maamuzi na utungaji wa sera zinazowahusu.

Amesema,  baraza hilo litasaidia kutumia uzoefu wa manusura kuboresha mifumo ya ulinzi, upatikanaji wa haki na sera zinazolenga kutokomeza ukatili wa kijinsia na kingono.

Maonyesho hayo yanalenga kutoa nafasi kwa jamii na mamlaka za kisheria kusikiliza uzoefu wa manusura, kuongeza uelewa na kuchukua hatua madhubuti za kuzuia na kutokomeza ukatili wa kijinsia na kingono nchini.