Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Haki za Binadamu Zilindwe Kuanzia Vituo vya Polisi

Imewekwa: 22 Sep, 2023
Haki za Binadamu Zilindwe Kuanzia Vituo vya Polisi

Na William Mabusi – WKS Busega

Wananchi wa Kata ya Nyashimo wameliomba Jeshi la Polisi chini kulinda haki za binadamu na kuzuia ukatili wa kijinsia kuanzia vituo vya Polisi wakibainisha kwamba kuna unyanyasi mwingi wakati wa kukamata mtuhumiwa na wakati mtuhumiwa akizuiliwa kwenye vituo hivyo.

Malalamiko hayo yametolewa mbele ya Timu inayotekeleza Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia Wilayani Busega kwenye mkutano uliofanyika Kata ya Nyashimo tarehe 19 Septemba, 2023.

Bila kutaka majina yao kutajwa wamesema “yapo matukio ya mtuhumiwa aliyeonesha ushirikiano wakati wa kukamatwa kwake na bado akaambulia kipigo lakini pia mtuhumiwa kula chakula mbele ya ndoo ya kujisaidia ni ukiukwaji wa haki za binadamu” Aidha, wananchi hao wamelalamikia Madawati ya Jinsia na Watoto kutokuwa na Afisa mwanaume kusikiliza kero za akina baba wakisema huo ni ukatili wa kijinsia.

Akijibu tuhuma hizo, Afisa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Busega Bi. Neema Zebedayo  amesema matukio ya watuhumiwa kupigwa na Askari yaripotiwe na hatua sitahiki zitachukuliwa. Aidha, aliwahakikishia wananchi kwamba Madawati ya Jinsia na Watoto yana maofisa wanawake na wanaume kusikiliza kero za wananchi.

Akitoa elimu ya ukatili wa kijinsia na namna ya kukabiliana nao, ametoa wito kwa wananchi kufika Dawati la Jinsia na Watoto au kutumia namba 116 ambayo ni bure kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia na matukio mengine yasiyofaa kwenye jamii, “kunyamazia matukio ya ukatili wa kijinsia ni kufanya ukatili zaidi,” alisema.

Kampeni hiyo inafanyika kwenye Halmashauri zote za Mkoa wa Simiyu kwa siku kumi baada ya kuzinduliwa na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana tarehe 18 Septemba, 2023 Mjini Bariadi.