Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Igunga Kupata Jengo Jipya la Mahakama ya Wilaya

Imewekwa: 06 Feb, 2024
Igunga Kupata Jengo Jipya la Mahakama ya Wilaya

Na William Mabusi – WKS Dodoma

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema Serikali imepanga kujenga jengo la Mahakama ya Wilaya ya Igunga katika mwaka wa fedha 2024/25.

Dkt. Chana amesema hayo tarehe 06 Februari, 2024 Bungeni alipokuwa anajibu swali la Mbunge wa Igunga  Mhe. Nicholaus George Ngassa aliyetaka kujua lini Serikali itajenga jengo la Mahakama ya Wilaya ya Igunga.

“Igunga ni moja ya Wilaya ambazo hazina jengo la Mahakama ya Wilaya kwa muda mrefu. Kwa sasa Mahakama ya Wilaya inafanya kazi ndani ya jengo moja na Mahakama ya Mwanzo Igunga mjini, jengo ambalo lilijengwa kwa ajili ya Mahakama ya Mwanzo. Kwa kuzingatia Mpango wa ujenzi wa Mahakama, jengo la Mahakama ya Wilaya ya Igunga linatarajiwa kujengwa katika Bajeti ya Mwaka 2024-25.” Amesema.