Jamii ya Kimasai Kata ya Engaruka Wafurahia Msaada wa Kisheria

Mwenyekiti wa Kijiji cha Chairerendeni, Kata ya Engaruka, Wilayani Monduli Mkoani Arusha Bw. Imani Lemayani amemshukuru Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa msaada wake wa kisheria alioupeleka Wilayani Monduli, akisema umekuwa na tija kubwa kwa wananchi waliokuwa na migogoro mbalimbali ya kisheria.
Lemayan pia ameeleza kuwa timu ya wanasheria wanaotekeleza Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa kisheria ya Mama Samia, wametoa elimu kubwa kwa wananchi wa kijiji chake kuhusu masuala mbalimbali ya kisheria na haki za binadamu, jambo ambalo litasaidia jamii kujitambua na kuepukana na migogoro mbalimbali ihusuyo sheria.
Kampeni ya Kitaifa ya msaada wa kisheria ya Mama Samia inatekelezwa kwenye Kata na Wilaya zote za Mkoa wa Arusha kwa siku 10, kampeni ambayo imeasisiwa na kufadhiliwa na Rais Samia huku ikiratibiwa na Wizara ya Katiba na Sheria na kufikia sasa imekwishatekelezwa kwenye mikoa 23, lengo likiwa ni kufikia Mwezi Mei, 2025 iwe imewafikia wananchi wa mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.