Kabudi Aanza Kazi Rasmi MoCLA
Na Hyasinta Kissima – WyKS
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (Mb) ameanza kazi rasmi kwa kuwataka Watumishi wa Wizara hiyo kuwa kinara katika kutekeleza kwa vitendo falsafa ya 4R ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Prof. Kabudi ameyasema hayo tarehe 20 Agosti, 2024 wakati akizungumza na Watumishi katika hafla fupi ya makabidhiano ya Ofisi yaliyofanyika Ofisi za Wizara Mtumba jijini Dodoma.
"Tunapozungumzia 4R za Rais Samia Reconciliation (maridhiano), Reforms (mabadiliko), Resilience (ustahimilivu) na Rebuilding (kujenga upya) sisi tunapaswa kuwa kinara. Tunapozungumzia Reconciliation hatuangalii makundi ya Kisiasa pekee. Wapo Wakulima na Wafugaji ambao nao wanahitaji upatanisho.Yapo mambo ya kijamii, uchumi, utamaduni ambayo yanahitaji upatanisho. Tunapokwenda kutoa Msaada wa Kisheria tunapatanisha watu, tunafanya usuluhishi, tunasaidia watu kuelewa haki zao. Tunafanya Reform katika Sheria mbalimbali. Hivyo inatubidi kuhakikisha tunayasimamia haya kikamilifu." Alisema.
Aidha, Waziri Kabudi amesema kuwa anamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumwamini ambapo ameahidi kufanya kazi kwa bidii na kwa uaminifu.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi Ofisi, Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye ndiye aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana alisema Wizara ya Katiba na Sheria ilimpatia ushirikiano wa kutosha katika kuhakikisha anatimiza majukumu yake ipasavyo na kuwataka watumishi waendeleze mshikamano huo kwa Prof. Kabudi ambaye hii ni mara yake ya tatu kuongoza Wizara hiyo na amesema katika Wizara ya Maliasili na Utalii yapo maeneo mengi ambayo Wizara hiyo inashirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria hususan katika kusimamia Haki za Binadamu.