Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Kamati Yaidhinisha Bajeti ya Mahakama kwa Mwaka wa Fedha 2024/25

Imewekwa: 18 Mar, 2024
Kamati Yaidhinisha Bajeti ya Mahakama kwa Mwaka wa Fedha 2024/25

Na William Mabusi – WKS Dodoma

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti ikiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Daniel Sillo imepokea na kuidhinisha Makadirio ya bajeti ya Mhimili wa Mahakama kwa mwaka wa fedha 2024/25 ikiwa ni ongezeko la asilimia 10.67 kutoka bajeti ya mwaka wa fedha 2023/24 huku wakiutaka mhimili huo kuongeza Mahakama zinazotembea (Mobile Courts) na kupanua wigo wa matumizi ya mfumo wa Unukuzi na Tafsiri wa Mwenendo wa Mashauri ya Mahakama (Transcription and Translation System - TTS).

Akisoma Makadirio ya bajeti hiyo mbele ya Kamati tarehe 18 Machi, 2024 Ofisi za Bunge Dodoma, Mtendaji Mkuu wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel ameyataja baadhi ya maeneo ya kipaumbele kuwa ni pamoja na Kuongeza Mobile Courts sita, Kuendelea kupunguza mrundikano wa mashauri mahakamani (backlogs), Kukamilika ujenzi wa Vituo sita Jumuishi vya Utoaji Haki (ICJ). Aidha, bajeti hiyo inalenga kuimarisha usimamizi wa utendaji kazi na kuimarisha mafunzo kwa watumishi.

Akichangia kwenye kikao hicho Mjumbe wa Kamati hiyo Mhe. Dkt. Charles Kimei amesema Mahakama iweke mkakati wa kuendelea kusimika mfumo wa TTS kwenye Mahakama zingine nchini kwani hadi sasa ni Mahakama 11 tu zinazotumia mfumo huo.

Katika uhitaji wa Mahakama zinazotembea (Mobile courts) Dkt. Kimei amesema "Mobile court ziongezeke basi mbona bado ni zile zile mbili, aidha Kamati ingependa kupata mrejesho wa kuwepo kwa Mobile Wagon Court baada ya treni ya mwendokasi (SGR) kuanza kufanya kazi.”

Akijibu hoja hiyo Mtendaji Mkuu wa Mahakama amesema Mahakama imefikia makubaliano na Wizara ya Uchukuzi na kwamba Mobile Wagon Courts zitaanza kutumika pale treni ya mwendo kasi itakapoanza kufanya kazi. Na kuhusu kusimikwa kwa mfumo wa TTS amesema mfumo unaposimikwa kwenye Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Mahakama zote zilizoko katika Kituo hicho kuanzia Mahakama ya Mwanzo hadi ya Rufani huunganishwa na mfumo.

Akitoa shukrani zake kwa Kamati, Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ameihakikishia Kamati kwamba kazi zote ambazo zimeombewa fedha zitatekelezwa kwa ufanisi mkubwa “Mahakama za Mwanzo 72 zilizoombewa fedha zitajengwa kwa mwaka wa fedha 2024/25 lengo likiwa kuwa na Mahakama za Mwanzo karibu kila Kata ingawa haziwezi kuwa Kata zote kwani Kata zingine hasa za mjini ziko karibu karibu ila kwa Wilaya ni ndoto za Wizara kuona kila Wilaya inakuwa na Mahakama.

Katika taarifa yake kwenye kikao hicho, Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaendelea kutoa fedha kwa Mahakama ili kuhakikisha shughuli za mhimili huo muhimu za utoaji haki zinatekelezwa kama ilivyopangwa, ikiwemo kugharamia Mahakama mpya zilizokamilika kujengwa.

“Mahakama ndiyo taasisi inayokimbiliwa na wengi katika kutoa haki hivyo Serikali huwa inaihudumia kadri inayotakiwa na hata ikitokea dharula ambayo itapelekea kasi ya kupeleka fedha kwenye Mahakama kupungua ni lazima hata wao (Mahakama) watakubaliana na Serikali kwamba sababu hiyo ni ya msingi na ilipashwa itekelezwe kwanza.” Alisema Mhe. Mwigulu