Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Kamati Yaridhishwa na Utekelezaji wa Miradi

Imewekwa: 17 Mar, 2024
Kamati Yaridhishwa na Utekelezaji wa Miradi

Na William Mabusi – WKS Dodoma

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Joseph Mhagama amesema Kamati imeridhishwa na matumizi ya fedha iliyoidhinishwa Bungeni kutekeleza miradi mbalimbali ndani ya Wizara ya Katiba na Sheria na Taasisi zake na kwamba Kamati iko tayari kupokea na kujadili makadirio ya Bajeti ya Wizara hiyo mwaka wa fedha 2024/25.

Dkt. Mhagama ameyasema hayo wakati Kamati ilipotembelea Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kilichopo jengo la Makao Makuu ya Mahakama Jijini Dodoma, tarehe 17 Machi, 2024, siku ya mwisho kwenye ziara ya Kamati kutembelea miradi ambayo pesa yake ilipitishwa na Bunge kwenye bajeti ya mwaka 2023/24.

Katika ziara hiyo Kamati imeoneshwa jinsi mfumo wa Kunukuu na Kutafsiri (Transcription and Translation System - TTS) unavyofanya kazi ya kunukuu na kutafsiri mwenendo wa uendeshaji wa mashauri ya Mahakama na taarifa yake kuchapishwa kwa muda mfupi sana yaani ndani ya saa 12.

”Kazi iliyokuwa inafanywa na Majaji ya kumsikiliza mtu halafu anaandika kwenye karatasi ilikuwa inachukua muda mrefu sana kuandaa taarifa za mienendo ya mashauri ya Mahakama. Lakini kwa kutumia mfumo huu hukumu  inatoka ndani ya saa 12 haya ni mapinduzi makubwa kwenye eneo la utoaji haki katika nchi yetu.” amesema Dkt. Mhagama na kuongeza kuwa ”Bunge liko tayari kujadili bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2024/25 tukiamini bajeti ya mwaka 2024/25 itahusisha kuimarisha mifumo kama hii kwenye Mahakama zetu.”

Pia Dkt. Mhagama amesema, ”endapo mfumo huu utafungwa kwenye Mahakama zote nchini kuanzaia Mahakama za Mwanzo hadi za Rufani tutakuwa tumesogeza huduma ya upatikanaji wa haki kwa uhakika, kwa ufanisi na kwa wakati kwa watanzania walio wengi. Aidha, kutapunguza muda wa kusubiri hukumu na yule anayetaka kukata rufaa baada ya hukumu, hivyo natoa wito kwa Mahakama kuhakikisha mfumo unafungwa kwenye Mahakama zote nchini na niiombe Serikali itangaze mfumo huu kwa nchi zote zinazotumia lugha ya Kiswahili ili ziutumie na hapo nchi itakuwa imejiingizia mapato.”

Katika ziara hiyo Kamati ilifanya majaribio ya mfumo huo katika kuendesha shughuli za Bunge, jaribio ambalo lilionesha kuwa mfumo unaweza kutumika Bungeni kunukuu vikao vya Bunge vya siku ambapo mazungumzo yote yatarekodiwa kisha kutafisiriwa katika kuandaa taarifa mbalimbali kwa muda mfupi ikiwemo uandaaji wa hansadi. Dkt. Mhagama akasema Bunge litaendelea kusoma mfumo huo ili lione jinsi gani unaweza kuboreshwa ukaweza kutumika Bungeni kusaidia Bunge kufanya kazi za uwakilishi wa wananchi, utungaji sheria na usimamizi wa Serikali kwa ufanisi.

Akiongea katika ziara hiyo Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ameishukuru Kamati kwa pongezi walizotoa kwa Wizara kwa kuridhishwa na utekelezaji wa miradi ambayo Kamati imetembelea.

“Katika ziara hii Kamati imepata fursa ya kutembelea Mahakama ya Mwanzo Mahenge, Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Njombe, Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Ruvuma, na leo mmejionea wenyewe kukamilika kwa kituo hiki Jumuishi cha Utoaji Haki na mfumo wa TTS, nikuhakikishie Mhe. Mwenyekiti ushauri na mapendekezo ambayo Kamati yako imetoa tutaendelea kuyafanyia kazi. Kwetu sisi hii ni bahati kupata fursa ya kuonesha maboresho makubwa yanayofanywa na Wizara ikiwa ni jitihada za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.”