Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Kamati za Usalama Arusha Zatakiwa Kufanya Kazi Kama Timu

Imewekwa: 16 Mar, 2025
Kamati za Usalama Arusha Zatakiwa Kufanya Kazi Kama Timu

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Paul Makonda, amewataka wajumbe wa Kamati za Usalama mkoani humo kufanya kazi kama timu, pamoja na kuwa na vipaumbele vya miradi ya kimkakati inayopaswa kujivunia kwa viongozi wa kitaifa wanapotembelea mkoa huo.

Makonda amezungumza hayo wakati akifunga mafunzo ya elimu ya uraia na utawala bora kwa wajumbe wa Kamati ya Usalama wa Mkoa wa Arusha pamoja na kamati za usalama za Wilaya ya Arusha na Arumeru, yaliyoandaliwa na Wizara ya Katiba na Sheria, tarehe 13 Machi, 2025.

Amesema Arusha kama mkoa unapaswa kuwa na mambo makubwa yanayoweza kufanywa kipaumbele kwa viongozi wa Kitaifa hususan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, hivyo ni muhimu kamati za usalama kutambua kila mradi unaotekelezwa na ukubwa kishwa kuainisha ile yenye kuuzika kwa wananchi na viongozi wakuu.

Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango na Bajeti wa Wizara ya Katiba na Sheria, Maria Kwambaza, ameeleza lengo la kutoa mafunzo hayo kuwa ni pamoja na “kuboresha utendaji kazi wa viongozi wa Serikali za Mitaa kwa kuzingatia haki za binadamu, utawala bora, demokrasia na kudumisha ulinzi na usalama.”

Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Elisante Ulomi, mkufunzi wa mafunzo hayo kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, amesema moja ya mambo muhimu ya Kamati za Usalama Arusha kupata mafunzo hayo na kufundishwa kuhusu Ulinzi na Usalama, ni kutokana na mkoa huo kuwa wa kimkakati pamoja na miradi mikubwa inayotekelezwa yenye masilahi makubwa kwa taifa ukiwamo Uwanja wa Mpira.

“Ni mkoa ambao una vivutio vingi vya utalii lakini pia una watalii wengi ambao wanatoka nje ya nchi kuja Arusha.” Amesema ACP Ulomi.

Mratibu wa mafunzo hayo kutoka Wizra ya Katina na Sheria Wakili wa Serikali Mkuu Bi. Joyce Mushi, amesema “katika mafunzo mada mbalimbali zimetolewa na mada kubwa ambayo imewahusu washiriki hawa ni mada ya ulinzi na usalama, washiriki wamepokea mafunzo haya na wameahidi kwamba watakwenda kuyafanyia kazi kwasababu ni mafunzo ambayo yanawagusa moja kwa moja.”