Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Kampeni ya Mama Samia Kupunguza Mabango ya Malalamiko - RC Tanga

Imewekwa: 09 Apr, 2025
Kampeni ya Mama Samia Kupunguza Mabango ya Malalamiko - RC Tanga

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Balozi Batilda Buriani amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha Kampeni ya Msaada wa Kisheria kwani itapunguza mabango ya kero za wananchi wakati wa ziara na mikutano mbalimbali.

Balozi Batilda Buriani ameyasema hayo Aprili 7, 2025 Jijini Tanga wakati akifungua kikao kazi cha wataalam watakaotoa Huduma ya Msaada wa Kisheria wakati wa utekelezaji wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia katika Mkoa wa Tanga.

Amesema, "Kikao kazi hiki kinachowahusisha Wataalam watakaokwenda uwandani kwa ajili ya kutoa Huduma za Msaada wa Kisheria, kitawajengea uwezo watekelezaji wa kampeni katika ngazi ya Halmashauri ili waweze kuainisha maeneo yenye uhitaji mkubwa na mapendekezo ya mkakati wa kuwafikia Wananchi hivyo, nawasisitiza kuzingatia kufanya kazi kwa weledi ili muweze kufanikisha dhamira ya Mhe. Rais ya kumsaidia mwananchi."

Balozi Batilda ameweka bayana kuwa katika Mkoa wa Tanga migogoro mingi zaidi ipo katika maeneo ya ardhi, mirathi, unyanyasaji wa kijinsia na ukatili wa watoto ambapo suala ya ulawiti kwa watoto wa kike na kiume limekua sugu na jambo la kushangaza linafanywa na watu wazima wenye heshima zao, twendeni tukashughulikie migogoro hiyo, tunahitaji Taifa lenye maadili".

Ameongeza kuwa kumekuwa na ucheleweshwaji wa utatuzi wa kero na migogoro mbalimbali kwakuwa hakukuwa na fursa ya kuwakutanisha pamoja wataalam wanaohusika katika utatuzi wa migogoro kama ilivyofanyika katika utekelezaji wa Kampeni hii ambayo inahusisha Wanasheria, Maafisa Ardhi, Maafisa Ustawi, Maafisa Maendeleo ya Jamii, Afisa wa Dawati la Jinsia na Msajili Msaidizi kutoka dawati la msaada wa kisheria.

Aidha, Mkurugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Ester Msambazi amesema malengo ya kikao kazi hicho ni kuwakutanisha watekelezaji wa Kampeni ili kubadilishana uzoefu na kujua maeneo ya kuzingatia zaidi wakati wa utoaji huduma.

Msambazi amesema Mkoa wa Tanga utazindua Kampeni tarehe 8 Aprili, 2025 katika viwanja vya Tangamono na kutekelezwa katika Halmashauri 11 kwa muda wa siku tisa.