Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Kampeni ya Mama Samia yatatua mgogoro Berege.

Imewekwa: 08 May, 2023
Kampeni ya Mama Samia yatatua mgogoro Berege.

Na George Mwakyembe & Lusajo Mwakabuku – WKS Mpwapwa

Mama Samia Legal Aid Campaign inayoendelea mkoani Dodoma imekuwa msaada mkubwa katika kutatua matatizo mbalimbali katika jamii mbali ya kutoa elimu ya kisheria, pamoja na msaada wa kisheria. Hilo limethibitika katika kijiji cha Berege kata ya Berege Wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma baada ya kampeni hii kuwakutanisha wanakijiji na Mwenyekiti wao ambapo kwa takribani miaka mitatu hapakuwa na mahusiano mazuri hali iliyopelekea kushindwa kufanyika kwa vikao vya maendeleo katika Kijiji hicho.

Akiongea mbele ya mkutano wa hadhara ulioitishwa na wataalam kutoka Wizara ya Katiba na Sheria pamoja washirika wa Azaki zisizo za kiserikali, mwenyekiti wa Kijiji hicho bwana Zebedayo Mchiwa alishukuru kwa ujio wa kampeni hiyo kwani umeweza kutibu mgogoro huo ambao ulipelekea kutoweka kwa hali ya amani na maelewano kati ya uongozi na wanakijiji.

“Kumekuwepo na tofauti kubwa zilizopelekea migongano kati ya mwakilishi wa wananchi na mimi lakini kwa kuwa wote tupo hapa kwa ajili ya kuhudumia wananchi na mimi ni kiongozi, nakubali kujishusha ili tuzike tofauti zetu kuanzia leo ili tuweze kuendelea kufanya kazi kwa pamoja kwa wananchi wetu badala ya kuendekeza tofauti zetu.” Alisema bwana Mchiwa.

Mgogoro huo umesababisha kutokuwepo kwa vikao vya kijiji kwa takribani miaka mitatu hatimaye umefikia kikomo baada pande zote mbili zilizokuwa zinapingana kukubali kumaliza tofauti zao na kutanguliza maendeleo ya nchi mbele hali ambayo imeshuhudiwa na wataalam wanaotoa msaada na elimu ya kisheria waliofika katika Kijiji hicho. Baada ya pande zote mbili kukubaliana Mwenyekiti wa kijiji alitangaza kufanya mkutano wa kijiji siku ya Jumatano tarehe 10 Mei, 2023 kujadili maendeleo ya kijiji.

Mwenyekiti wa kijiji hicho ndugu Sila Zebedayo Mchiwa ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea kampeni ya msaada wa kisheria pamoja na elimu ya sheria kwani wamejifunza mengi pamoja na kupata uelewa mpana wa masauala ya sheria.

“hii ni fursa nzuri sana kwa wananchi wangu wa kata ya Berege kuweza kuyafahamu mambo mbalimbali yanayohusiana na sheria hivyo ni vyema tukaitumia vizuri nafasi hii katika kupata elimu lakini pia tuitumie kutatua migogoro midogo midogo ambayo si lazima ifike mahakamani.” Alimalizia bwana Mchiwa.