Kituo Jumuishi Temeke Kinabeba Dhamira ya Rais Katika Uboreshaji wa Huduma za Haki Nchini
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini Septemba 26, 2024 alitembelea katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, ambapo katika ziara hiyo Naibu Waziri amejionea na kufurahishwa na huduma jumuishi zitolewazo kituoni hapo.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mhe. Sagini amesema kuwa Sekta ya Mahakama Nchini imeendelea kupiga hatua kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika kuboresha huduma za utoji haki katika Vituo Jumuishi vya Mahakama Nchini.
"Uwepo wa Kituo hiki hapa Temeke unaonesha dhamira ya dhati aliyonayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha jamii inapatiwa ufumbuzi wa matatizo mbalimbali na haki inatendeka kwa kila mtu na kwa wakati. Niwapongeze pia kwa kuwa katika kipindi cha miaka mitatu tangu kuanzishwa kwa Kituo hiki mmeweza kufanya tathmini na kupata taarifa halisi kuwa malengo ya kuanzishwa kwa Kituo hiki yamefikiwa kwa asilimia mia moja hii ni hatua kubwa." Alisema Sagini.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel amesema kuwa Kituo Jumuishi cha Temeke ni miongoni mwa vituo sita Nchini Tanzania ambapo kwa ujumla wake vituo hivyo vinagharimu kiasi cha Shilingi bilioni 51.45 vituo viwili vikiwa katika Mkoa wa Dar es Salaam wilaya ya Temeke na Kinondoni, Vituo vingine vinne katika Mkoa wa Morogoro, Dodoma, Mwanza na Arusha ambapo katika Kituo hicho Wananchi kati ya 800 hadi 1000 huudumiwa kwa siku.
Awali Naibu Waziri Sagini alitembelea katika maeneo mbalimbali ya utoaji huduma na kuzungumza na Wananchi waliokuwa wakipatiwa huduma ambapo Wananchi hao walikiri wazi kuwa Kituo hicho kimekuwa na Msaada kwao kwa kuwapatia uelekeo wa masuala yanayohusu Ndoa, Mirathi, Msaada wa Kisheria na pia kimewapa Wananchi nafuu kubwa kwani huduma zote hutolewa bila malipo.