TANZANIA YAWASILISHA TAARIFA YA MIFUMO YA ULINZI NA USTAWI WA MTOTO UN
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuimarisha mifumo ya kisera, kisheria na kitaasisi katika kulinda, kukuza na kutekeleza haki za mtoto, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Mtoto.
Hayo yamesemwa na Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Ofisi za Umoja wa Mataifa na Mashirika Mengine ya Kimataifa Geneva, Mhe. Dkt. Abdallah S. Possi, wakati akizungumza katika Kikao cha 101 cha Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Mtoto kinachoendelea jijini Geneva, ambapo Taarifa ya Sita ya Tanzania kuhusu utekelezaji wa Mkataba huo inajadiliwa.
Mhe. Dkt. Possi amesema Tanzania imechukua hatua mbalimbali katika kuimarisha ulinzi na ustawi wa mtoto, ikiwemo kutungwa kwa kanuni mbalimbali za utekelezaji wa Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009. Kanuni hizo, zilizotungwa kati ya mwaka 2011 na 2016, zinahusu ulinzi wa mtoto, uasili, ajira kwa mtoto, uendeshaji wa mashauri ya watoto katika Mahakama za Watoto pamoja na makazi ya watoto. Aidha, amesema watoto walishirikishwa katika uandaaji wa Taarifa ya Sita ya Tanzania pamoja na wadau mbalimbali wa haki za mtoto.
Ameeleza kuwa Tanzania imepiga hatua katika maeneo ya afya na lishe, usajili wa vizazi, elimu na kuzuia vitendo vya ukatili dhidi ya watoto. Hata hivyo, amesema bado kuna changamoto zinazohitaji kushughulikiwa, ikiwemo mila na tamaduni zinazoweza kuhatarisha haki na ustawi wa mtoto, kama vile ukeketaji.
Mhe. Dkt. Possi amesema Tanzania itaendelea kukabiliana na changamoto hizo kwa kuimarisha ulinzi, uratibu, uelimishaji na utekelezaji wa mifumo ya kitaifa, ikiwemo MTAKUWA, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano na Asasi za Kiraia (CSOs), Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs), Wabia wa Maendeleo na wadau wengine. Amesema Tanzania itaendelea kutimiza wajibu wake wa kulinda na kutekeleza haki za mtoto pamoja na kushirikiana na Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Mtoto.