Kupiga Vita Rushwa ni Jukumu Letu Sote – Mhe. Pindi Chana.
Na George Mwakyembe – WKS Dodoma.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema kuwa uwepo wa vitendo vya rushwa kunaifanya Serikali kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo, kushindwa kuwahudumia wananchi, miradi ya maendeleo kushindwa kufanyika au kufanyika kwa kiwango cha chini kutokana na fedha zinazotengwa kutekeleza miradi hiyo kuingia katika mikono ya watu wachache.
Mhe. Chana ameyasema hayo alipokuwa akizindua Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa yaliyofanyika tarehe 03 Desemba, 2023 kwenye Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.
“Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu ni fursa nzuri ya kujitafakari tulikotoka na tunakokwenda katika jitihada za kuimarisha uchumi pamoja na uboreshaji wa huduma kwa wananchi.” Alisema.
Akitoa salaam, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Jaji Mstaafu Mhe. Mathew Mwaimu amesema Tanzania imepiga hatua kubwa sana katika kusimamia masuala ya haki za binadamu na hii inadhihirishwa na Mhe. Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa mstari wa mbele katika kupinga vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu ikiwemo unyanyasaji, rushwa na ukatili wa kijinsia.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na wananchi kutoka mikoa mbalimbali nchini yakiambatana na mbio ndefu na fupi zilizoitwa Sepesha Rushwa Marathoni zikiwa na lengo la kupinga vitendo vya rushwa nchini. Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni “Zingatia Maadili, Utu, Uhuru na Haki kwa watu wote kwa Maendeleo ya Endelevu.”
Maadhimisho hayo yanaadhimishwa sambamba na maadhimisho ya miaka 75 ya Tamko la Haki za Binadamu (Universal Declaration of Human Rights) ambayo huadhimishwa kila tarehe 10 Desemba ya kila mwaka hivyo siku hiyo ndiyo itakuwa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa.