Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Mahakama Ijiandae Kukabiliana na Wimbi la Kesi za Akili Bandia (Artificial Intelligence).

Imewekwa: 28 Jan, 2024
Mahakama Ijiandae Kukabiliana na Wimbi la Kesi za Akili Bandia (Artificial Intelligence).

Na William Mabusi – WKS Dodoma.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani Dkt. Tulia Ackson ameitaka Mahakama ya Tanzania kujiandaa kukabiliana na waathirika wa matumizi ya akili bandia wakati ikiendelea kuboresha matumizi ya TEHAMA katika kutoa haki.

Dkt. Tulia ameyasema hayo alipokuwa akihutubia kwenye uzinduzi wa Maadhimisho ya Wiki ya Sheria yaliyofanyika Kitaifa Jijini Dodoma tarehe 27 Januari, 2024 ambapo yeye alikuwa Mgeni Rasmi. Kabla ya uzinduzi huo Dkt. Tulia aliongoza matembezi yaliyoanzia Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma na kuishia Viwanja vya Nyerere Square.

“Kwa kuwa sehemu kubwa ya mfumo unatumia akili bandia naiona hatari ya wadanganyifu kutumia teknolojia hiyo kugombanisha watu au kupotosha nia nzuri ambayo tunaitamani kwa matumizi ya akili bandia. Hivyo naomba mjiandae kukabiliana na kesi za waathiriwa na matumizi ya akili bandia. Kwani kwa kutumia akili bandia mtu anaweza kufanywa kafanya tukio na kumbe kiuhalisia siye, mdanganyifu anaweza kutumia sauti ya mtu anayefahamika kusikika kwenye maneno ambayo anataka yamfikie mtu fulani au umma fulani.” Alisema baada ya kuzindua mfumo wa Unukuzi na Tafsiri wa Mienendo ya Mashauri (Transcription and Translation- Software – TTS).

Awali akimkaribisha Mgeni Rasmi, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, alisema mfumo wa Unukuzi na Tafsiri wa Mienendo ya Mashauri unatumia akili bandia au mnemba (Artificial intelligence) na umefundishwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza cha kisheria na kimahakama kwa mazingira ya Tanzania ili usaidie kufanya unukuzi (transcription) na pia kutafsiri (translation) katika lugha ya Kiswahili au Kiingereza.

Mfumo huo unawapunguzia Majaji na Mahakimu kazi kubwa waliyokuwa wanaifanya ya kuandika kwa mkono mienendo ya mashauri na kisha kuchapwa na Makatibu Mahsusi na hivyo kupelekea wananchi kupata haki kwa wakati hasa wanapokuwa wanataka kukata rufaa.

Mfumo wa TTS umeshafungwa na kuanza kutumika kwa awamu ya kwanza katika Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki vya Arusha, Dodoma, Mwanza Kinondoni, Temeke na Morogoro, Mahakama Kuu Dar es Salaam, Bukoba na Musoma.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana hakuweza kushiriki ufunguzi wa maadhimisho hayo kwa kuwa yuko kwenye majukumu mengine nje ya Dodoma.

Maadhimisho ya Wiki ya Sheria yameanza tangu tarehe 24 Januari 2024 kwenye Viwanja vya Nyerere Square ambapo Wadau wa utoaji haki wanatoa elimu ya sheria, msaada wa kisheria na kuzungumza na wananchi mambo mbalimbali yahusuyo umuhimu wa haki kama kigezo muhimu cha ustawi wa taifa. Maadhimisho ya Wiki ya Sheria yatahitimishwa tarehe 01 Februari, 2024.