"Majaji na Waendesha Mashtaka Wajengewe Uwezo Kuendesha Mashauri Dhidi ya Biashara Haramu ya Binadamu" - Maswi

Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Eliakim Maswi amesema Nchi ya Tanzania imefanya jitihada mahususi katika kupambana na usafirishaji haramu wa Binadamu ikiwemo marekebisho ya Sheria mbalimbali na adhabu kali kwa watuhumiwa wa biashara hiyo, licha ya uhaba wa rasilimali fedha na uwezo mdogo wa Wataalam wa kada mbalimbali wakiwemo Majaji na Waendesha Mashtaka wenye Elimu ya Mapambano dhidi ya biashara hiyo.
Bw. Maswi amesema hayo katika kikao cha kubadilishana uzoefu wa mbinu zinazoweza kutumika dhidi ya Usafirishaji haramu wa Binadamu kilichowakutanisha wataalam kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ujumbe kutoka Nchini Marekani wanaohusika na mapambano dhidi ya usafirishaji haramu wa Binadamu kilichofanyika tarehe 30 Oktoba, 2024 katika ukumbi wa Wizara Mtumba jijini, Dodoma.
Maswi ameeleza kuwa ili kuweza kuendana na wakati na kudhibiti biashara hiyo, Majaji na Waendesha Mashtaka ni miongoni mwa kada zinazotakiwa kujengewa uwezo ambapo takwimu zinaonesha kuwa Waendesha Mashtaka wanne waliopo kwenye kikosi kazi cha mapambano hayo ndiyo waliojengewa uwezo kuhusiana na Mapambano hayo.
"Biashara ya Usafirishaji Haramu wa Binadamu ni biashara inayowahusisha watu wenye fedha, hivyo hata mapambano yake yanahitaji uwezo wa kifedha. Kwa upande wa Wizara ya Katiba na Sheria yapo maeneo ambayo Wataalam wake wanahitaji kujengewa uwezo wakiwemo Majaji na Waendesha Mashtaka ili kuweza kuwa na uelewa mpana na kuendesha mashauri yanayohusiana na biashara hiyo." Alisema Katibu Mkuu.
Kwa upande wake Ofisa kutoka Ofisi inayoshughulika Utokomezaji na ufuatiliaji wa biashara ya usafirishaji haramu wa Binadamu kutoka Nchini Marekani Bw. Adam Blakeman amesema kuwa Nchi ya Tanzania ni miongoni mwa Nchi zilizopiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya biashara hiyo ukilinganisha na Nchi nyingine barani Afrika.