MAKAMU WA RAIS AZINDUA MAONESHO YA KILIMO; WIZARA YA KATIBA NA SHERIA YASHIRIKI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango leo Agost 1, 2025 amefungua maonesho ya wakulima, wafugaji na wavuvi (Nanenane) yanayofanyika Kitaifa katika Viwanja vya Nzuguni mkoani Dodoma yakiwa yamebeba kauli mbiu ya “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025”
Dkt. Philip Mpango ametoa rai kwa viongozi kutambua wajibu wa kutekeleza Dira ya Taifa 2050 na mipango ya maendeleo ya sekta ya kilimo ambayo imedhamiria kuongeza kasi ya ukuaji wa kilimo hadi kufikia asilimia 10 kwa mwaka, ifikapo 2030 na kuendelea.
Aidha Wizara ya Katiba na Sheria imeshiriki maonesho hayo wakiwa wamejipanga kutoa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa huduma za Msaada wa Kisheria kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia.
Huduma nyingine ni pamoja na Kutoa elimu kwa umma kuhusu utawala bora na uraia hususani katika kipindi hiki cha kuelekea katika Uchaguzi Mkuu, Kutoa elimu kwa umma kuhusu haki za msingi za binadamu na wajibu, Kutoa elimu kwa wadau mbalimbali kuhusu uangalizi wa utajiri wa asili na maliasili za nchi na Kutoa elimu kwa umma kuhusu shughuli mbalimbali zinazo tekelezwa na Wizara pamoja na taasisi zilizo chini yake.