Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Mawaziri wa Sheria Kutoka Jumuiya ya Madola Kutiririka Tanzania – Dkt. Chana

Imewekwa: 07 Feb, 2024
Mawaziri wa Sheria Kutoka Jumuiya ya Madola Kutiririka Tanzania – Dkt. Chana

Na William Mabusi – WKS Dodoma

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Pindi Chana amesema maandalizi ya Tanzania kupokea Mawaziri wa Sheria wa nchi 56 Wanachama wa Jumuiya ya Madola wakiambatana na Maofisa wao Waandamizi yamefikia mwishoni na hivyo Mawaziri hao kuanza kutiririka Nchini kuanzia Machi 04, 2024.

Dkt. Chana ameyasema hayo leo tarehe 07 Februari, 2024 alipofanya mkutano na Wandishi wa Habari Bungeni Jijini Dodoma kueleza maandalizi ya Mkutano huo.

“Maandalizi ya Mkutano huo yanafanywa na Wizara ya Katiba na Sheria kwa upande wa Tanzania Bara na Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola una dhima isemayo Technology and Innovation: How Digitization Paves the Way for the Development of People-Centered Access to Justice, yanendelea vizuri.” Amesema.

Mikutano hii huwa na vigezo vingi vya kuangalia kama vinazingatiwa kabla kuruhusiwa kufanyika katika nchi husika. Amevitaja baadhi ya vigezo hivyo kuwa ni pamoja na utawala bora wa nchi husika na kuzingatiwa kwa masuala ya amani. Mkutano wa mwisho wa Mawaziri wa Sheria kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola ulifanyika Mauritius mwaka 2022.

Mkutano huo utakaofanyika Unguja-Zanzibar kuanzia tarehe 04 mpaka 08 Machi, 2024 Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, sio tu utaitangaza nchi yetu katika anga za kimatifa bali utatumika kama chanzo cha mapato ya fedha za kigeni. Aidha, mkutano huo utakuwa fursa kwa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati kufanya biashara zao eneo la mkutano.