Mhe. Ndumbaro Aungana na Wanyarwanda Kumbukizi ya Mauaji ya Kimbari

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro Aprili 7, 2025 Jijini Dar es Salaam ameungana na raia wa Rwanda waishio nchini katika tukio la kuomboleza Miaka 31 ya mauaji ya kimbari yaliyotokea nchini Rwanda mwaka 1994 dhidi ya kabila la Watusi.
Akizungumza katika tukio hilo, Mhe. Ndumbaro amesisitiza umuhimu wa kujikumbusha kuhusu tukio hilo la kihistoria, akisema kuwa tunapoadhimisha miaka hii 31, ni vyema kutafakari chanzo cha mauaji haya ili kuhakikisha kuwa tukio kama hili halijirudii.
"Mauaji ya kimbari ni kosa kubwa kwa mujibu wa Sheria za Kimataifa na ni uhalifu dhidi ya binadamu. Wakati tunasherehekea miaka hii 31, ni muhimu kujikumbusha kwamba nini kilitokea, nini kilisababisha, na tunajifunza nini kutoka kwa tukio hili la huzuni," amesema Mhe. Ndumbaro.
Ameongeza kwamba matamshi ya kibaguzi na kichochezi ni baadhi ya silaha zinazoweza kuchochea vurugu na kuleta madhara makubwa kwa jamii.
Kwa upande wake, Balozi wa Rwanda nchini Tanzania, Mhe. Jenerali Patrick Nyamvumba, amezungumzia changamoto kubwa ilizopitia Taifa hilo wakati wa mauaji hayo, huku akieleza maendeleo makubwa ambayo Rwanda imefanya tangu wakati huo.
Amesisitiza kuwa licha ya maafa yaliyotokea, Rwanda imeweza kujikwamua kutokana na ujasiri na juhudi kubwa za kuleta amani na maendeleo katika nyanja mbalimbali, akitaja elimu, afya, na uchumi kama mifano ya mafanikio hayo.
"Tunajivunia hatua kubwa ambazo Rwanda imefikia baada ya mauaji ya kimbali. Ingawa tulikumbana na changamoto kubwa, leo hii tunaona Nchi yetu ikikua kwa haraka," amesema Balozi Nyamvumba.
Katika kuadhimisha siku hii Balozi Nyamvumba amesisitiza umuhimu wa umoja na mshikamano katika kujenga jamii zinazoheshimu haki za binadamu, na kutoa wito kwa watu wote duniani kushirikiana ili kuzuia na kupambana na matukio ya mauaji ya kimbari.