Migogoro ya Ndugu Kudhulumiana Ardhi Yakithiri Kampeni ya Mama Samia Legal Aid Meru

Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia "Mama Samia Legal Aid" imebaini uwepo wa migogoro mingi ya ardhi katika Halmashauri ya Meru Wilayani Arumeru inasababishwa na ndugu kudhulumiana mali za urithi ikiwemo ardhi.
Migogoro hiyo imebainika kujitokeza kwa wingi kwenye zoezi la uzinduzi wa Kampeni ya Samia Legal Aid katika eneo la Malula katika Kata ya King'ori, Halmashauri ya Meru, Wilayani Arumeru leo Machi 31, 2025.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, aliyekuwa Mgeni Rasmi wa uzinduzi huo Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Amir Mkalipa amesema migogoro hiyo imekuwa ikisababishwa na wananchi wengi kutokuwa na mazoea ya kuandika wosia.
"Ukiona mwananchi amefika ofisini ana malalamiko yake basi ujue ni mgogoro kati ya ndugu kwa ndugu na kubwa inasababishwa na ndugu kudhulumiana ardhi ambapo idadi kubwa ya wanaodhulumiwa ni Wanawake" amesema Mkalipa.
Amesisitiza kuwa, ili kuepuka migogoro ya aina hiyo, Wananchi wa Meru wanatakiwa kujifunza umuhimu wa kuandika wosia pindi wakiwa hai na kuwataka wanaoachiwa mirathi hiyo kufuata taratibu za Kisheria ili kuepuka migogoro hiyo.
"Kwa kuwa huku kwenu imebainika migogoro mingi inatokana na dhuluma ya mali hasa ardhi, leo mtapewa elimu ya mirathi na namna ya kuandika wosia, tunataka hii migogoro iishe kabisa, lakini timu ya Msaada wa Kisheria itatoa elimu kuhusu masuala ya ndoa," amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria kutoka Wizarani Ester Msambazi amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi ili waweze kunufaika na Elimu ya Msaada wa Kisheria ambayo imekuwa na mwitikio mkubwa na imeweza kutatua migogoro ya wananchi katika maeneo mbalimbali.
"Niwaombe wananchi wa Meru na Arusha kuitumia fursa hii ya uwepo wa Mawakili hawa ili kuweza kuleta matatizo ya Kisheria yaliyokuwa yanawatatiza. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa gharama za kuhakikisha Wataalam hawa wanawafikia na mnatatuliwa kero zenu. Wapo Mawakili wenye ubobezi katika mambo mengi kama Ardhi, Ndoa, Mirathi na Kazi." Amesema Mkurugenzi Ester.