Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Mkuu wa Wilaya awanyooshea kidole watumishi wa ardhi

Imewekwa: 21 Jun, 2023
Mkuu wa Wilaya awanyooshea kidole watumishi wa ardhi

Na William Mabusi – WKS Shinyanga

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Bi. Johari Musa Samizi amewataka watumishi wa ardhi kufanya kazi kwa kufuata haki na taratibu za kazi wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku katika kuwahudumua wananchi ili kuepuka kusababisha migogoro ya ardhi nchini.

Bi. Samizi ameyasema hayo wakati timu zilizokuwa zinatekeleza kampeni ya kitaifa ya Mama Samia Legal Aid Campaign kwenye Manispaa ya Shinyanga na Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga zilipofika ofisini kwake tarehe 21 Juni, 2023 kutoa mrejesho wa utekelezaji wa kampeni hiyo iliyokuwa inatekelezwa mkoani humo kwa siku kumi kuanzia tarehe 11 hadi 20 Juni 2023.

Mtumishi anafanya anachojua na siyo kwamba hajui anachofanya, anajua kabisa hapa nachakachua na hapa sitendi haki lakini anafanya tu, mwananchi mnyonge ndiye anayeumizwa zaidi labda mwananchi huyo awe mnyonge na awe mbishi kweli kweli. Nawaasa watumishi wenzangu tuwatendee haki wananchi kwani wao ndio wanafanya twende kazini, wasipokuwepo hatuna kazi.” Alisema Bi Samizi.

Katika siku kumi za kutekeleza kampeni hiyo katika Mkoa wa Shinyanga ambapo yeye mwenyewe alishiriki kwa nyakati tofauti, elimu ya sheria imetolewa, wananchi wamepewa huduma ya msaada wa kisheria na baadhi ya migogoro kupatiwa ufumbuzi.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amesema, “Kampeni hii imetupunguzia kazi, migogoro mingi imetatuliwa na hiyo mingine inayotakiwa kufuatiliwa tutaifuatilia, maeneo mengi nilikuwa nikienda nakutana na migogoro tu lakini kwa kampeni hii tumefanya jambo.”

Ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata elimu ya sheria na huduma ya msaada wa sheria hata baada ya kampeni hiyo kumalizika wilayani mwake, Bi. Samizi amaesema atajipanga na Wataalam wake katika kila ziara atakayofanya kwenye Kata ataambatana nao ili watoe elimu kwanza kabla ya yeye kuhutubia.

Akiongelea mamlaka iliyonayo Serikali za Vijiji kuhusu ardhi Bi. Samizi amesema, “Serikali ya kijiji ndiyo yenye mamlaka ya ardhi, pale inapotokea viongozi hao wametoa ardhi ya Kijiji kwa sababu yoyote ile watoe taarifa kwa wananchi wao ili kuepusha migogoro.

Awali, timu ya MSLAC iliyokuwa inatekeleza kampeni hiyo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga ilikutana na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Shinyanga Dkt. Nuru Yunge kumpa mrejesho wa kampeni hiyo huku ikilalamikia mwitikio mdogo wa akina mama kwenye mikutano ya hadhara, changamoto ambayo amesema itafanyiwa kazi kwenye matukio mengine yatakayofuata.