Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

MSLAC Yarejesha Viwanja Viwili Alivyoporwa Mwananchi

Imewekwa: 23 Sep, 2023
MSLAC Yarejesha Viwanja Viwili Alivyoporwa Mwananchi

Na William Mabusi – WKS Bariadi

Mgogoro uliodumu kwa miaka miwili kati ya Bi. Mboje Masanja Ndahile Mkazi wa eneo la Imalilo Kata ya Bunamhla na Halmashauri ya Mji wa Bariadi ambao haukumpa matumaini ya kupata viwanja vyake viwili umetatuliwa na Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid Campaign - MSLAC) kwa siku tatu na mama huyo kurejeshewa viwanja vyake.

Jitihada za kupata viwanja hivyo zilikuwa zimegonga mwamba kwani kila alipokuwa anafuatilia aliambiwa Serikali imechukua viwanja hivyo ili kupanga mji na hakukuwa na namna nyingine ya kuvipata. “niliposikia kuna kongamano la sheria na watu wanasaidiwa nilikuja na kuonana na wataalam wa sheria akiwepo kiongozi wenu na akaagiza nipate viwanja vyangu na kweli nimevipata hizi hapa barua za kurejeshewa viwanja hivyo.” Alisema huku akionesha nakala hizo alipokuwa amerudi kushukuru timu ya MSLAC iliyokita kambi kwenye viwanja vya Stendi ya zamani Mjini Bariadi tarehe 23 Septemba, 2023.

Bi. Mboje alifika viwanja hivyo na kuonana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo tarehe 20 Septemba, 2023 aliyekuwa viwanjani hapo kujionea mwenyewe utekelezaji wa Kampeni hiyo inayoendelea kutekelezwa kwenye Halmashauri zote sita Mkoani Simiyu. Baada ya kuridhishwa na maelezo yake Bi. Makondo aliagiza watumishi wa Kitengo cha Ardhi wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi kuhakikisha mama huyo anapatiwa haki yake.