MSLAC Yatwishwa Mgogoro wa Kijiji cha Bumangi

William Mabusi – WyKS Butiama
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria na Mbunge wa Butiama Mhe. Jumanne Sagini amewatwisha Wataalam wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia – MSLAC mgogoro wa kijiji cha Bumangi kilichoko Kata ya Muriaza Wilayani Butiama baada ya wanakijiji hao kunyang’anywa eneo lao la soko.
Uamuzi huo umefikiwa wakati wa mkutano wa hadhara kati ya Kijiji cha Bumangi na Mhe. Sagini Agosti 07, 2024. Katika mkutano huo wananchi walilalamika kunyang’anywa eneo ambalo hata ramani ya Kijiji inaonesha eneo hilo lilikuwa limetengwa kutumika kama soko.
“Hizi ni zama za utawala wa haki. Haikubaliki mtu kutumia uwezo na ushawishi wake kumnyima mtu mwingine haki, na hiki ndicho kinachoonekana kwenye mgogoro huu, mtu katumia uwezo wake kuchukua eneo la Kijiji, nakuhakikishieni wananchi kuwa wataalam wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria watashughulikia mgogoro huu hadi haki ipatikane,” amesema.
Akiongelea kuhusu mgogoro huo Mwenyekiti wa Kijiji cha Bumangi Bw. Itonge Kyamung'aro amesema eneo hilo limechukuliwa tangu mwaka 2017 na jitihada za uongozi wa Kijiji kuokoa eneo hilo zimekuwa zikigonga mwamba.