Nchi ikitawaliwa na rushwa haiwezi kufikia malengo: Bi. Makondo
Na William Mabusi – WKS Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo amezitaka Taasisi za Serikali na Sekta Binafsi kuweka mazingira ya kuzuia rushwa, kuepuka na kutokomeza vitendo vya rushwa nchini ili kuliwezesha taifa kufikia malengo mbalimbali iliyojiwekea katika kuleta maendeleo nchini.
Bi. Makondo ameyasema hayo alipokuwa akihutubia kwenye Jukwaa la Kitaifa la Wadau wa juhudi dhidi ya rushwa tarehe 04 Desemba, 2023 Jijini Dodoma lililo hudhuriwa na Wadau kutoka Serikalini, Sekta Binafsi na Viongozi wa Dini ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu nchini. Siku ya Maadili na Haki za Binadamu nchini Tanzania ni jumuisho ya siku mbili za Kimataifa ambazo ni siku ya Kupambana na Rushwa na Siku ya Haki za Binadamu.
“Sote tunaelewa rushwa ni adui mkubwa wa maendeleo, nchi ikitawaliwa na rushwa taifa haliwezi kufikia malengo ililojiwekea katika nyanja mbalimbali. Aidha, rushwa inakiuka haki za binadamu kwa kuwa ulaji rushwa unapokonya haki za binadamu na kusababisha huduma mbalimbali kutowafikia wananchi kwa wakati,” alisema.
Siku ya Maadili na Haki za Binadamu ambapo kwa mwaka huu uzinduzi wake umefanyika tarehe 3 Desemba, 2023 inaadhimishwa sanjari na shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanyika kwa Jukwaa la Kitaifa la wadau wa juhudi dhidi ya rushwa, Maadhimisho ya Wiki ya huduma kwa jamii yatakayofanyika kwenye viwanja vya Nyerere Square kuanzia tarehe 5 hadi siku ya kilele Desemba 10, 2023 ambapo wadau wa Serikali na Mashirika yasiyo ya Kiserikali yanayojihusisha na masuala ya maadili na haki za binadamu watatoa huduma mbalimbali, watajibu maswali kuhusu haki katika nyanja ya maadili, kuzuia na kupambana na rusha, utawala bora na haki za binadamu.
Ametaja shughuli nyingine kuwa ni utoaji wa elimu kupitia Vyombo mbalimbali vya Habari ili kuendelea kuuhabarisha umma juu ya umuhimu wa kuzingatia maadili, kutokujihusisha na rushwa na kuzingatia haki za binadamu.
Kwenye mjadala uliofanyika kwenye Jukwaa la Kitaifa la Wadau wa Juhudi dhidi ya rushwa washiriki wamesisitiza elimu kuhusu maadili mema kuendelea kutolewa ili jamii ijikite katika kufanya mambo mema vile vile wamewataka Watanzania kusimamia mali ya umma kama vile wanavyosimamia mali zao wenyewe kwa faida ya kizazi chetu kijacho na maendeleo ya nchi. Maadhimisho ya siku ya Maadili na Haki za Binadamu kwa mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo “Zingatia maadili, utu, uhuru na haki kwa watu wote kwa maendeleo endelevu.”