Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Ndumbaro atangaza neema kwa Waandishi Ruvuma

Imewekwa: 19 Jul, 2023
Ndumbaro atangaza neema kwa Waandishi Ruvuma

Na Lusajo Mwakabuku – Ruvuma

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro ameahidi kutoa zawadi nono kwa Waandishi watatu wa habari wa mkoa wa Ruvuma watakaofanya vizuri katika ushiriki, upashaji habari  na uhamasishaji wakati wa utekelezaji wa kampeni ya Kitaifa ya msaada wa kisheria inayojulikana kama Mama Samia Legal Aid Campaign mkoani humo. 

Waziri Ndumbaro ameyasema hayo tarehe 19/07/2023 mjini Songea Mkoani Ruvuma wakati akifungua mafunzo yaliyojikita kuwajengea uwezo Waandishi wa Habari katika maeneo ya utafiti, uchambuzi na upashaji habari kwa masuala yanayohusu vitendo vya ukatili wa kijinsia. Mafunzo hayo ya siku mbili  yalitolewa kwa Wahariri na Waandishi wa Habari 25 kutoka Vyombo mbalimbali vya Habari mkoani humo. Mhe Waziri aliwakumbusha washiriki kuhusu nafasi yao kwenye jamii wanayoisha na kuwaasa kufanya kazi kwa weledi na kutumia ubunifu katika kutimiza majukumu yao kwa maslahi mapana ya Taifa.

“Ninatamani sana mtoke katika mafunzo haya mkiwa watu mliobadilika, na nawaagiza watumishi wa ofisini kwangu kuhakikisha kwamba wale watu watatu watakaofanya kazi yao vizuri hususan katika kampeni hii ya Mama Samia wanapewa zawadi, na zawadi hii yaweza kuwa fedha taslimu, nishani na pia kualikwa kushiriki katika mikoa mingine ambayo kampeni hii inaendelea kutekelezwa.” Ndumbaro alieleza.

Aidha, Mheshimiwa Ndumbaro aliwataka Waandishi kuhakikisha wanaandika habari ambazo zinakuwa na mwendelezo ili waweze kuzitumia kalamu zao katika kuibadilisha jamii na sio kubaki kuripoti matukio ambayo yanakuwa hayasaidii jamii kutokana na kukosekana kwa uwajibikaji wa wale walioshutumiwa.

“Kukosekana kwa uendelevu wa Habari, hili ni eneo jingine ambalo limeonesha udhaifu jinsi habari zetu zinavyopelekwa kwa jamii. Mwandishi anaripoti mtu kakamatwa kawekwa ndani stori imeisha, hatujui kilichotokea baada ya kukamatwa na hatua zilizochukuliwa baada ya  hapo.” Aliongeza Ndumbaro.