Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Ongezeni juhudi katika utoaji elimu ya sheria kwa umma: Gekul

Imewekwa: 23 Jun, 2023
Ongezeni juhudi katika utoaji elimu ya sheria kwa umma: Gekul

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul amewataka watumishi wa Tume ya Kurekebisha Sheria   kuongeza juhudi katika suala la utoaji elimu kwa umma kuhusiana na masuala mbalimbali ya kisheria ili jamii iweze kuzitambua Sheria zilizopo nchini na kuwasaidia kuzitumia hususan pale ambapo wanapotaka kufahamu haki zao juu ya  jambo husika.

"Kiu kubwa ya jamii ipo kwenye elimu, sheria tunazo nyingi sana zimetungwa lakini jamii zetu haizifahamu sheria hizo na wengi wanateseka kupata haki zao kupitia sheria kwasababu hawana elimu ya kutosha ya kuzijua sheria hizo." 

Mhe. Gekul amebainisha hayo wakati akizungumza na Watumishi wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania alipokuwa katika ziara yake ya kutembelea Tume hiyo iliyofanyika tarehe 22 Juni, 2023 Jijini Dodoma.

Naibu Waziri Gekul yupo katika ziara ya kutembelea Taasisi mbalimbali zilizopo ndani ya  Wizara ya Katiba na Sheria kwa lengo la kufahamiana, kufahamu  majukumu yao, mafanikio na changamoto mbalimbali zinazoikumba taasisi hizo.

Aidha, Naibu Waziri amewataka watumishi wa Tume ya Kurekebisha Sheria kutoa elimu ya sheria kwa umma kupitia nyanja mbalimbali zikiwemo Vyombo vya Habari, Mitandao ya Kijamii na Semina mbalimbali ili kuwasaidia wananchi kuzijua sheria za nchi na  kupata haki zao kupitia sheria hizo.