Orodha ya Watoa Huduma za Msaada wa Kisheria Nchini Iandaliwe - Waziri Chana
Hyasinta Kissima-WKS
Waziri wa Katiba na Sheria Mheshimiwa Dkt. Balozi Pindi Chana akiwa ameambata na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Jumanne Sagini ameagiza kuandaliwa kwa orodha "Directory" ya Watoa Huduma za Msaada wa Kisheria Nchini, ili kuwawezesha Wananchi kuwatambua wakati wanapohitaji Msaada wa Kisheria.
Waziri Chana ameyasema hayo tarehe 10 Juni, 2024, jijini Dodoma wakati akipokea taarifa ya utekelezaji wa Mafunzo kwa Wasajili Wasaidizi wa Watoa Msaada wa Kisheria kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria Bi. Ester Msambazi, mafunzo ambayo yaliyofanyika jijini Mbeya tarehe 6 -7 Juni, 2024 na kufunguliwa na Waziri mwenye dhamana.
"Tunawapongeza Idara ya Huduma za Msaada wa Kisheria kwa kufanikisha mafunzo hayo na kuendelea kuwajengea uwezo Wasaidizi hao katika kuhakikisha Wizara inawafikia Wananchi katika maeneo mbalimbali na wanahudumiwa na Wataalamu wenye uelewa wa masuala mtambuka ya Kisheria. Jambo la muhimu nasisitiza tuandae orodha "Directory" ya Watoa Huduma za Msaada wa Kisheria Nchini ili tuweze kuwatambua katika kila Mkoa." Alisema Waziri Chana
Ikumbukwe kuwa Lengo la uwepo wa Watoa Huduma za Msaada wa Kisheria kwa kushirikiana na Wataalamu wa Wizara ya Katiba na Sheria ni kusaidia kusikiliza na kushughulikia changamoto za Kisheria zilizopo kwenye maeneo yao hususani changamoto za masuala ya Ardhi, Wosia na Mirathi, Ndoa, Matunzo kwa Watoto na Migogoro mingineyo inayohitaji msaada wa Kisheria.