Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Serikali Kuanzisha Kituo cha Kudumu Kushughulikia Malalamiko

Imewekwa: 28 Jan, 2024
Serikali Kuanzisha Kituo cha Kudumu Kushughulikia Malalamiko

Na William Mabusi – WKS Dodoma

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi amesema Serikali inaangalia uwezekano wa kuanzisha kituo cha kudumu Makao Makuu ya nchi kushughulikia kero za wananchi.

Dkt. Feleshi ameyasema hayo alipoongea na Wanahabari baada ya kutembelea mabanda kwenye viwanja vya Nyerere Square kunakofanyika maonesho ya Wiki ya Sheria tarehe 28 Januari, 2024.

“Pamoja na maadhimisho ya Wiki ya Sheria kila mwaka, matumizi ya kurasa za maoni kwenye tovuti, simu za kupokelea maoni na sasa kuna Mama Samia Legal Aid Campaign ambayo hadi sasa imetekelezwa kwenye mikoa sita Tazania Bara tungeweza kusema sasa mifumo ya kupokelea maoni na malalamiko inatosha, lakini unaona malalamiko yapo, bado wananchi wana kero, mfano migogoro ya ardhi na mirathi.” Amesema na kuongeza “Hivyo Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wadau wengine tutaangalia uwezekano wa kuanzisha kituo cha kudumu kama njia ya nyongeza ya kutoa huduma za kisheria kwa maana ya kuelimisha umma masuala ya sheria, kupokea malalamiko na kutoa huduma za kisheria.”

Maadhimisho ya Wiki ya Sheria kwa mwaka 2024 yamezinduliwa tarehe 27 Januari, 2024 na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Dkt. Tulia Ackson na hitimisho ni tarehe 01 Februari, 2024.