SERIKALI YAAHIDI MABADILIKO YA SHERIA KUKUZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA NA UCHUMI WA KIDIJITALI
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Katimba amesema Serikali inaendelea kufanya mapitio ya sheria mbalimbali Nchini ili kuhakikisha kuwa zinaendana na mabadiliko ya kiteknolojia na mahitaji ya sasa ya kiuchumi, ikiwemo utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050 iliyoanza kutekelezwa mapema hii leo.
Akizungumza wakati alipotembelea banda la Tume ya Marekebisho ya Sheria katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Jijini Dar Es Salaam, Mhe. Katimba amesema kazi kubwa ya tume hiyo ni kupitia upya sheria ili kuziwezesha taasisi na wananchi kunufaika na mageuzi ya kidigitali yanayoendelea duniani.
Amesema katika mwaka mpya wa bajeti 2026/2027, Serikali imeweka msukumo mkubwa katika kupunguza matumizi ya fedha taslimu na kuhamia kwenye mifumo ya kidigitali, hatua inayohitaji sheria imara zinazowezesha mabadiliko hayo katika sekta zote.
“Tunaenda kwenye matumizi yasiyo ya fedha taslimu, lazima sheria zetu ziweze kuwezesha hayo.”
Katika hatua nyingine Mhe. Katimba amesema kuwa serikali itaendelea kushirikiana na Tume ya Marekebisho ya Sheria pamoja na wadau wengine kuhakikisha mfumo wa sheria unakuwa rafiki kwa maendeleo ya kidigitali na uchumi wa kisasa.