Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

WIZARA YA KATIBA NA SHERIA YAHIMIZA UTATUZI WA MIGOGORO KWA NJIA MBADALA

Imewekwa: 02 Jul, 2026
WIZARA YA KATIBA NA SHERIA YAHIMIZA UTATUZI WA MIGOGORO KWA NJIA MBADALA

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Katimba, amesisitiza umuhimu wa matumizi ya njia mbadala za utatuzi wa migogoro (Alternative Dispute Resolution – ADR), kwa kuwa njia hizo zinasaidia kufikiwa kwa maridhiano na kupatikanika kwa suluhu kwa amani baina ya pande mbili tofauti na mashauri ya mahakamani ambayo mara nyingi huacha upande mmoja ukiwa mshindi na mwingine kushindwa.

‎Mhe. Katimba ametoa msisitizo huu wakati alipotembelea banda la Wizara pamoja na Taasisi zilizo chini yake zinazoshiriki katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere (Sabasaba) jijini Dar es Salaam 1 Julai, 2026, ambapo pia alishiriki kutoa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi waliofika katika banda la wizara.

‎Mhe. Katimba amesema pamoja na Mahakama kuwa ndiyo mhimili wenye jukumu la kusimamia utoaji wa haki kwa mujibu wa Katiba, Serikali inaendelea kuhamasisha matumizi ya usuluhishi na njia mbadala za kutatua migogoro ili kupunguza migongano na kujenga maridhiano miongoni mwa wananchi.

"Sisi tunaamini kuwa migogoro mbalimbali inayojitokeza inaweza kutatuliwa pia kwa njia mbadala tofauti na kwenda mahakamani, njia ya usuluhishi ni njia ambayo inazifanya pande mbili zenye migogoro ziridhiane kwa amani, kuwa na  suluhu ya kudumu na kuzifanya zote kuwa na ushindi tofauti na kukinzana Mahakamani ambapo upande mmoja huibuka mshindi." amesema Mhe. Katimba

Aidha, Mhe. Katimba, amewaalika wananchi kutembelea banda la Wizara ili waweze kupata huduma mbalimbali za kisheria ikiwemo elimu ya Uraia na Utawala Bora, Msaada wa Kisheria, utatuzi wa migogoro ya ndoa, ardhi, mirathi na matunzo ya watoto, masuala ya ukatili wa kijinsia, usuluhishi wa migogoro kwa njia mbadala pamoja na elimu ya usimamizi wa masuala yanayohusu utajiri asilia na maliasili za Nchi