Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Serikali Yaboresha Huduma za Haki Jinai kwa Njia ya TEHAMA

Imewekwa: 30 Jan, 2024
Serikali Yaboresha Huduma za Haki Jinai kwa Njia ya TEHAMA

Na Lusajo Mwakabuku - WKS Dodoma.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imeendelea kuonesha nia yake thabiti ya kuboresha upatikanaji haki kwa wakati kwa  kutoa vifaa vya TEHAMA vitakavyorahisisha huduma za Haki katika taasisi mbalimbali zinazohusika na masuala ya Haki Jinai.

Akikabidhi vifaa hivyo kwa niaba ya Serikali, Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Dkt. Pindi Chana amesema Serikali imeendelea kusimamia uwekaji wa mifumo na miundombinu ya TEHAMA thabiti ikiwemo kupata elimu ya masuala ya sheria, ufunguaji wa kesi, uendeshaji wa kesi, upatikanaji wa nyaraka za kesi na ushahidi, hukumu na maamuzi ya kesi na uwepo wa vyombo vya utoaji haki katika ngazi za kijamii na upatikanaji wa huduma za msaada wa kisheria.

Waziri Chana ameeleza hayo leo tahe 30 Januari 2024 Jijini Dodoma kwenye  hafla ya ugawaji wa vifaa vya TEHAMA vilivyonunuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita ambavyo ni Kompyuta, Seti za Video Conferencing, Printer na Vifaa vya Mtandao lengo ni kuziwezesha Taasisi za Haki Jinai kutoa huduma kwa wananchi kwa kutumia fursa za mifumo ya TEHAMA iliyojengwa.

Akisoma hotuba yake, Waziri Chana amesema Mahakama ya Tanzania imepatiwa Seti za kuendesha mashauri kwa njia ya Mtandao ambazo zitaharakisha uendeshaji wa mashauri na kupunguza mlundikano wa mashauri kwa Majaji na Mahakimu, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imepatiwa kompyuta ambazo zitarahisisha utendaji na matumizi wa mfumo wa kushughulikia majalada ya Mashtaka ili kupunguza mlundikano wa majalada ya upelelezi na kuongeza kasi ya upatikanaji wa haki jinai.

Kwa upande wa Gereza la Msalato na Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe-Sehemu ya Isanga zimepatiwa vifaa vya TEHAMA vitakavyowezesha uendeshaji wa mashauri pamoja na matumizi ya huduma za kisheria kupitia mifumo iliyopo kwa lengo la kuleta maboresho na haki za wafungwa na mahabusi na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mkoani Njombe, Magereza ya Ludewa na Njombe Mjini yatafungwa vifaa hivyo vya kisasa ili kuwezesha na kurahisisha uendeshaji wa mashauri pamoja na upatikanaji wa hukumu kwa wakati.

Waziri Pindi Chana ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejizatiti katika kuimarisha masuala ya utoaji na upatikanaji haki nchini kwa kuhakikisha Taasisi za Haki Jinai zimejenga mifumo mizuri ya TEHAMA ambayo inarahisisha upatikanaji wa taarifa na huduma za kisheria kwa wananchi kwa wakati  bila urasimu na kuepuka rushwa kwani haki iliyocheleweshwa ni haki iliyokataliwa.

Moja ya majukumu makubwa ya Wizara, ni kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati bila kujali dini, umbali au hali yoyote ya mtu.  Katika kufanikisha hilo, Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na mifumo imara ya utoaji na upatikanaji wa haki kulikopelekea kutoa kipaumbele cha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwani matumizi ya Teknolojia yatawapunguzia wananchi muda na gharama za kushughulikia masuala ya kisheria na badala yake watajikita zaidi katika shughuli za kiuchumi na kimaendeleo.