Sheria za Uangalizi wa Utajiri Asili na Maliasilia za Nchi Kuhuishwa

Na William Mabusi – WKS Dodoma
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amepokea taarifa ya maandalizi ya rasimu ya Mkakati wa mwaka 2024 – 2029 wa utekelezaji wa Sheria za Uangalizi wa utajiri asili na Maliasilia za nchi Sura 449 na 450.
Mkakati huo wenye lengo la kuhakikisha kuwa uvunaji na matumizi ya utajiri asili na Maliasilia za nchi unazingatia maslahi ya Taifa na Maendeleo endelevu ya wananchi, umewasilishwa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Uangalizi wa Utajiri Asili na Maliasilia za Nchi DCP Neema Mwanga, tarehe 24 Juni, 2024 ofisi za Bunge Dodoma.
Mkakati wa awali wa utekelezaji wa sheria tajwa wa mwaka 2019 umemaliza muda wake mwaka 2021/22. Mkakati wa sasa ni Jumuishi na utatekelezwa na Wizara, Idara na Taasisi zinazojihusisha na masuala ya utajiri asili na Maliasilia za nchi. Aidha, Mkakati huo utazingatia misingi ya Sheria tajwa pamoja na Sera na Sheria zingine ambazo ni msingi wa umiliki na udhibiti wa utajiri asili na maliasilia.