Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Tekelezeni kwa Ukamilifu Mfumo wa Utoaji Msaada wa Kisheria

Imewekwa: 01 Feb, 2024
Tekelezeni kwa Ukamilifu Mfumo wa Utoaji Msaada wa Kisheria

Na William Mabusi – WKS Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameitaka Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na Wadau wengine kutekeleza kwa ukamilifu mfumo wa utoaji huduma ya msaada wa kisheria kwa wanachi hasa wanyonge kupitia Kampeni ya Kitaifa ya Mama Samia Legal Aid Campaign ili kuwatatulia migogoro mbalimbali wanayokabiliana nayo.

Dkt. Samia ameyasema hayo alipokuwa akihutubia kwenye kilele cha Siku ya Sheria nchini leo tarehe 01 Februari, 2024 kwenye viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma.

“Tunashukuru sana kwani kwenye mikoa sita ambako kampeni imetekelezwa imepokelewa vizuri kwa wananchi, na kwa jinsi ilivyopokelewa ni wazi kuwa kuna uhitaji mkubwa wa msaada wa kisheria hapa nchini. Naiagiza Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na Wadau wengine kutekeleza kwa ukamilifu mfumo wa utoaji msaada wa kisheria kwa mujibu wa sheria.” Amesema na kuongeza “Mazingira ya jamii yetu yalitulazimu kuanzisha programu hiyo ili wananchi wasio na uwezo kupitia kampeni hiyo wapatiwe msaada wa kisheria.”

Utekelezaji wa kampeni hiyo umesaidia kubaini maeneo yenye malalamiko makubwa ambayo ni pamoja na migogoro ya ardhi, mirathi, ukatili wa kijinsia, ndoa na matunzo kwa watoto.

Katika hatua nyingine Mhe. Rais amesisitiza juu ya matumizi ya kuamua kesi kwa njia mbadala, “tuweke kipaumbele katika kuamua kesi kwa njia ya usuluhishi, kwani pande zinazohusika zikifikia maridhiano huepuka mapingamizi mengi katika uendeshaji wa kesi mahakamani. Shauri linaloisha kwa njia ya usuluhishi haliachi makovu kwa wahusika kuchukiana na hivyo wahusika kubaki wakiendelea kushirikiana katika kazi.”

Mhe. Rais akatoa wito kwa Vituo vya Sheria na Shule ya Sheria kuongeza kasi ya kuandaa wataalam katika tasnia ya usuluhishi nchini, vile vile akaitaka Wizara Katiba na Sheria kukaa na Wadau wa usuluhishi kubainisha maeneo yanayotakiwa kufanyiwa kazi ikiwemo hitajio la kutunga Sera ya usuluhishi.

Awali akimkaribisha Mgeni Rasmi, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, amesema utashi wa kisiasa unaooneshwa na Mhe. Rais Dkt. Samia umechangia kuboresha haki na haki jinai nchini, akitaja mifano michache amesema kuundwa kwa Tume ya Haki Jinai, kuanza kwa Kampeni ya Mama Samia ya Msaada wa Kisheria ni miongoni mwa ishara za utashi wa Kiasa wa Mhe. Rais.

Kilele cha Siku ya Sheria kilitanguliwa na maadhimisho ya Wiki ya Sheria kote nchini ambako wananchi walihudumiwa kwa kupewa elimu ya sheria. Siku ya Sheria huashiria kuanza kwa mwaka mpya kwa shughuli za Mahakama nchini.