Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

Tuko Vizuri Kwenye Suala la Amani – Dkt. Chana

Imewekwa: 30 Jan, 2024
Tuko Vizuri Kwenye Suala la Amani – Dkt. Chana

Na William Mabusi – WKS Dodoma

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema dunia ina imani na amani iliyoko nchini amani ambayo inachagizwa na utawala wa sheria.

Dkt. Chana amesema hayo alipotembelea mabanda ya maoenesho kwenye viwanja vya Nyerere Square na baadaye kuongea na Wanahabari, tarehe 30 Januari, 2024 Jijini Dodoma.

“Dunia ina imani na Tanzania kuhusu haki za binadamu na utawala bora ndiyo maana mkutano mkubwa wa 77 wa haki za binadamu na watu ulifanyika Arusha mwishoni mwa mwaka 2023. Kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu hawaendi tu mahali popote, haiwezekani, bali mikutano yao hupelekwa nchi yenye amani, isiyokuwa na vita,” amesema Dkt. Chana.

Waziri Chana aliongeza kuwa ni kutokana na utulivu ulioko nchini, Tanzania inaandaa Mkutano mwingine mkubwa wa Mawaziri wa Sheria wa Nchi za Jumuiya ya Madola ambao utafanyika Zanzibar tarehe 04 – 08 Machi 2024. Mkutano ambao unategemewa kuhudhuriwa na Mawaziri wa Sheria wasiopungua hamsini na sita.

Dkt. Chana ametumia wasaa huo kumpongeza na kumshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuanzisha reforms mbalimbali  kwa nia ya kuendelea kuboresha mnyororo wa haki jinai nchini, ”Mhe. Rais ameunda Tume ya Haki Jinai ambayo imekuja na mapendekezo mengi ambayo yameanza kutekelezwa kama tulivyoelezwa kwenye banda la Wadau wa Haki Jinai, amekubali kufanyika kwa Kampeni ya Kitaifa ya kutoa msaada wa Kisheria iitwayo Mama Samia Legal Aid Campaign ili wananchi wanyonge wafikiwe kupewa elimu ya sheria na msaada wa kisheria, kutatuliwa changamoto mbalimbali za kisheria bure, kwa kweli Mhe. Rais amedhamiria kuipeleka Tanzania kwenye nchi ya asali na maziwa.” Alisema.

Maadhimisho ya Wiki ya Sheria yalizinduliwa rasmi tarehe 27 Januari, 2024 na Mhe. Dkt. Tulia Ackson Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na yatahitimishwa Siku ya Sheria tarehe 01 Februari, 2024 kwenye Viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma ambapo Mgeni Rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.