Tusiwalee Wahalifu Kwani Ukatili Huanzia Katika Ngazi ya Familia Dkt. Ndumbaro

Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro amesema ukatili wa kijinsia huanzia katika ngazi ya familia na sio serikalini, hivyo basi wananchi wasiwalee wahalifu bali wawafikishe katika vyombo vya sheria ili haki itendeke.
Dkt. Ndumbaro ametoa rai hiyo leo wakati akizindua kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC) mkoani Tanga ikiwa ni Mkoa wa 24 kufikiwa na kampeni hii.
Dkt. Ndumbaro amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan amemtuma kwa wananchi wa Tanga kwakuwa anaamini wana kiu ya kupata haki ili asipatikane mwananchi anayeonewa kutokana na unyonge.
Ameongeza kuwa viongozi wa dini pia wana wajibu wa kukemea vitendo vya ukatili na watumishi wa serikali wasijivute katika kushughulikia malalamiko ya vitendo vya ukatili kwani kumekuwa na taarifa za uzembe wa kuchukua hatua katika kesi hizo.
Kabla ya kuhitimisha hotuba ya uzinduzi wa kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC) kwa mkoa wa Tanga, Dkt. Ndumbaro ametoa msaada wa kisheria kwa vitendo kwa baadhi ya wananchi.
Naye Naibu Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii na Makundi maalum, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju amesema mkoa wa Tanga unaongoza kwa vitendo vya ukatili, kutokana na taarifa za mwaka 2024 matukio 497 yameripotiwa kutokea mkoani Tanga Kati ya matukio 7320 yaliyotokea nchi nzima.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Batilda Buriani amewataka wananchi mkoani Tanga kuchukia vitendo vya ukatili kwa watoto na kuacha kukimbilia kwa viongozi kuomba dhamana kwa watuhumiwa.
Amesema, "tabia ya kuwafuata viongozi ili kutaka dhamana kwa watuhumiwa wa vitendo vya unyanyasaji ikome, Tanga tunaheshimika kwa ukarimu na kushika imani katika dini zote tujitahidi takwimu mbaya za ukatili tuziondoshe".
Ameeleza kuwa migogoro mingi mkoani Tanga ni ya ardhi, ukatili wa kijinsia, ukatili wa watoto masuala ya ndoa na kampeni ya MSLAC inayozinduliwa leo itawahudumia wananchi katika Halmashauri zote 11 za Tanga kwa muda wa siku tisa.
Ummy Mwalimu Mbunge wa Tanga mjini amesema katika ofisi yake ya Mbunge amepokea malalamiko ya migogoro mingi ya ardhi, mirathi na masuala ya ndoa hivyo uzinduzi wa kampeni ya MSLAC imekuja wakati muafaka kusaidia kutatua migogoro hiyo.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Tanga Cde. Rajab Abdulrahman Abdallah amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameona wananchi wanavyokosa haki kwa kutokuwa na pesa za kugharamia wanasheria hivyo kampeni hii ni msaada kwa wanyonge.