Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Katiba na Sheria

“Ukikiuka Utii Wa Sheria Utaendelea Kuwa Mteja Wetu” Waziri Chana.

Imewekwa: 25 Sep, 2023
“Ukikiuka Utii Wa Sheria Utaendelea Kuwa Mteja Wetu” Waziri Chana.

Na George Mwakyembe – WKS Iringa. 

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Pindi Chana amekemea vikali vitendo vyote vya ukatili unaofanywa na baadhi ya watu katika jamii zetu na kuwakumbusha kuwa vyombo vya haki anavyovisimamia vipo imara na makini katika kuhakikisha kila mtanzania anaishi kwa amani na hivyo kuitunza tunu yetu ya amani tuliyojijengea kwa muda mrefu.

Waziri Chana ameyasema hayo tarehe 25 Septemba, 2023 alipokuwa akipokea taarifa ya utendaji kazi kwa Ofisi ya Mashtaka Mkoa wa Iringa pamoja na taarifa ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Mkoa wa Iringa ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kutembelea ofisi za taasisi zilizo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria.

Akitoa taarifa kwa Waziri Chana juu ya utendaji kazi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa Mkoa wa Iringa, Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Iringa Bw. Basilius Namkambe alisema kumekuwa na ongezeko la vitendo vya ukatili katika Mkoa wa Iringa hasa wakati wa mavuno ya pombe aina ya ulanzi.

“Vitendo hivi vimekuwa vikifanyika na hatua zimekuwa zikichukuliwa, changamoto katika hili imekuwa ni kutojitokeza katika kutoa ushahidi mahakamani wakati wa kuendesha kesi, na hii imekuwa changamoto kubwa sana kwa mkoa wetu wa Iringa na tayari kwa mwaka huu tuna kesi  za makosa ya kubaka 129  kati ya hizo 83  zimeshia mahakamani na  kesi 46 bado zinaendelea,” alisema Bw. Namkambe.

Akiongea baada ya kupokea taarifa hizo Mhe. Chana amewasihi watendaji hao kutokata tamaa ya kuwachukulia hatua kali wale wote wanaofanya vitendo vya ukatili na pia wale wanaokiuka sheria za nchi, “nchi hii ina amani na utulivu, anayejichukulia sheria mkononi basi achukuliwe hatua kali za kisheria” Alisema Mhe. Chana.

Pia Mhe. Chana alipokea taarifa ya utendaji kazi kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa Mkoa wa Iringa huku akiwapongeza watendaji hao kwa kuokoa kiasi cha shilingi bilioni 6 kutoka katika mashauri 28 yaliyokuwa yakiendelea mahakamani kwa kipindi cha nusu mwaka yaani kutoka Januari mpaka Septemba, 2023.

“Nawapongeza sana kwa kazi kubwa mliyofanya ya kuitetea pamoja na kuiwakilisha Serikali katika mashauri mbalimbali yaliyopo mahakamani na hatimaye kuokoa kiasi cha shilingi bilioni 6, hizi ni juhudi kubwa sana na fedha hizi zitatumika katika  miradi  ya maendeleo ya watanzania” Alisema Mhe. Chana.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Uratibu na Usimamizi wa Kesi ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Bw. Camilius Ruhinda amemshukuru Mhe. Chana kwa kufanya ziara katika ofisi hizo na kumwahidi kuendelea kutoa ushirikiano na Wizara katika mashauriano mbalimbali.