UZALENDO, WELEDI NA NIDHAMU YA HALI YA JUU NI VIPAUMBELE KATIKA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA

Utendaji kazi unaozingatia uzalendo katika utoaji huduma, weledi na nidhamu ya hali ya juu vimetajwa kuwa ni vipaumbele muhimu ambavyo watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria wanapaswa kuvizingatia katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ili kuongeza kasi ya mabadiliko ya kiutendaji.
Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Ndg. Eliakim Maswi ametaja vigezo hivyo Julai 29, 2025 wakati wa kikao kazi na watumishi hao ambapo alitoa tathmini ya utendaji kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 na kutoa mwelekeo kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Maswi aliongeza kuwa, Wizara imejipanga vema kuongeza kasi na ubunifu ili kufanikisha ongezeko la upatikanaji haki hususani maeneo ya vijijini, kupunguza mashauri yaliyopo mahakamani kupitia usuluhishi wa Migogoro kwa njia mbadala na kuboresha zaidi mifumo ya TEHAMA katika utoaji wa huduma mbalimbali.
Aidha amewataka watumishi wote kuwa na mtazamo chanya unaozingatia weledi ili wawe chachu ya mageuzi katika mfumo wa Sheria na utoaji haki nchini na kuwaoongeza kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka uliopita.
Katika kikao kazi hicho Katibu Mkuu alipokea tuzo na zawadi mbalimbali ambazo Wizara imezipokea kwa kipindi cha mwaka mmoja ikiwemo Tuzo ya Mshindi wa pili katika kundi la Wizara kwenye usimamizi wa Rasilimaliwatu, Tuzo ya mshindi wa kwanza wa uzingatiaji wa Sheria na miongozo ya TEHAMA (e-governmnent), Tuzo ya ushiriki wa Wizara katika utoaji wa elimu na huduma za sheria kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma na Tuzo ya mshindi wa kwanza katika kundi la Wizara zilizoshiriki maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (sabsaba).
Kwa upande wao watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria wamempongeza Katibu Mkuu Maswi kwa uongozi imara hususani katika kuboresha mazingira ya utendaji kazi, kuwajali watumishi pamoja na kuongeza vitendea kazi ambavyo vimewezesha kuongeza ufanisi katika kazi.
Naye Mwandishi Mwendesha Ofisi kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Mwanahamisi Gomo aliahidi kuongeza bidii katika kutekeleza majukumu ili kuhakikisha Wizara inafikia malengo na kuongeza tija kubwa kwa taifa.